Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Malemve, Kata Igongwa, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wamekimbia kijiji hicho wakihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kudaiwa kuhusika kuwashambulia kwa fimbo na mawe watu wawili na kusababisha vifo kwa kuwatuhumu kuhusika na wizi wa kuku ambapo tukio hilo lilitokea Januari 11,2024 majira ya saa 10 jioni.
Kufuatia tukio hilo Ofisa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhani Sarige amewaonya wakazi wa kijiji hicho waliojichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia na kusababisha vifo vya watu hao.
Onyo amelitoa lJanuari 16, 2024 wakati akitoa elimu kwa wanakijiji katika mkutano wa hadhara ambapo amewahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wale wote waliohusika na kitendo hicho ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Msiwakumbatie wahalifu, mtapata shida. tunaamini waliofanya hili tukio ni wachache ndio maana tunawahimiza wananchi mtupe ushirikiano,msiogope kuwataja wahalifu, wahalifu sio watu wazuri”ameeleza ACP.Sarige.
Kwa upande wake, Mtemi wa Sungusungu Kanda ya Ziwa Martine Mogani, amesikitishwa na kitendo cha mauaji ya watu wawili kwa kujichukulia sheria mkononi kilichofanywa na baadhi ya wanakijiji hao na kuwataka wale waliokimbia warejee kwenye makazi yao na kuendelea na shughuli za maendeleo wakati vyombo vya dola vikifanya kazi yake.
“Wanaume hawapo na mashamba sasa hivi hayalimiki, tunapoelekea ni wapi sasa?, kabla sijaja hapa kupitia viongozi wenu, niliwaomba watu wote waje wahudhurie kwenye mkutano huu ili warejeshewe imani zao kule zilikokimbilia zitoke warudi kwenye utaratibu waendelee kuishi na familia, hawa wakina mama sasa hivi wanalala na baridi,”amesema Mogani.
Naye Mrakibu wa Polisi (SP) Henry Mbilinyi kutoka Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza amewaasa wananchi hao kuishi kwa upendo kama maandiko matakatifu yanavyosema kwani ukiwa na upendo huwezi kumfanyia ubaya binadamu mwenzako.
Awali wananchi hao walipatiwa elimu ya kupinga na kuzuia vitendo vya ukatili kutoka kwa Mratibu wa Polisi Jamii Mkoa wa mwanza Jovitha Tibangayuka na kuwataka kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi waonapo vitendo hivyo.
Yunus Manyilizu ni miongoni wa akina mama katika Kijiji hicho ambaye amewataka wanaume wa kijiji hicho kuacha kujichukulia sheria mikononi kwani wamesababisha adha kubwa kwa wanawake wa kijiji hicho kwa kukosa huduma waliyokuwa wanaipata.
“Nalishukuru Jeshi la Polisi kutupatia elimu na tutayafanyia kazi yale yote tuliyo ambiwa kwa kuwaelimisha wale waliokimbia kijiji kwa sababu ya hofu,”amesema Lenatus Masele Kiongozi wa Sungusungu katika kijiji hicho.
Kwa upande wake, Polisi Kata wa Kata hiyo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Fortunata Sikanda amewasihi wananchi wa kijiji hicho kuzuia uhalifu kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kuliko kupambana na uhalifu kwani gharama ya kupambana ni kubwa kuliko kuzuia.
ACP Sarige amehitimisha mkutano huo kwa kuwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali ipo macho na haiwezi kuvumilia kitendo kilichofanywa na wanakijiji hao kwani Jeshi la Polisi litawasaka na kuwakamata wale wote waliohusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi