Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
SHERIA ya habari inayohusu kashfa kuwa jinai, inakulinda pale tu kauli hiyo inayoweza kutafsiriwa kuwa ya kashfa, imetolewa bungeni ama na rais, basi.
Lakini andishi lingine lolote ambalo kama mahakama itasema ni kashfa, hapo mwandishi anaingia kwenye jinai, sasa sheria ya namna hii ya kibaguzi, haiwezi kuwa rafiki kwa wanahabari.
Hayo ameyasema James Marenga, Wakili wa kujitegemea pia akiiwakilisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) akizungumza na wahariri wa Magazeti ya Mwananchi leo.
Wakili Marenga amekutana na Lilian Timbuka, mhariri wa habari Mwananchi pia Samuel Kamdaya, Mahariri wa Habari wa The Citizen kuzungumzia mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari nchini.
“Pamoja na kwamba mwandishi amelindwa katika kipengele hicho, lakini bado sheria hiyo hiyo haimpi kinga kama habari hiyo itakwaza viongozi wa juu. Unaweza kuandika ila inategemea itapokelewa vipi.”
“Ndani ya sheria hizo kuna maeneo mwandishi anaweza kujikuta anaingizwa mkenge hata kwa nia njema ya habari aliyoiandika kwa taifa lake. Ndio maana tumeona kuna kila sababu ya kufanyia maboresho,” amesema Wakili Marenga.
Pia amesema, kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.
“Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo.
“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasehma sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,” amesema Wakili Marenga.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa