Na Mwandishi wetu,Timesmajira
WAKILI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa, ametangaza mpango wa kufungua kesi ya Kikatiba akiiomba Mahakama itoe tamko kuwa tozo ya kuvuka Daraja la Kigamboni ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Wakili Majaliwa amesema kesi hiyo anaifungua kwa niaba ya wananchi wa kigamboni ambao wamekuwa wakitumia juhudi mbalimbali za kutafuta suluhisho la kero hiyo kushindikana, hatua ambayo imepelekea kubeba mzigo mkubwa wa kifedha kwa kulipa kodi mara mbili.
Wakili Majaliwa amesema mfumo wa sasa wa utozaji tozo hizo unakiuka Kanuni ya Tozo za Barabara ya mwaka 1985 (The Road Tolls Fees Regulations, 1985) pamoja na Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta (The Road and Fuel Tolls Act), ambazo hazielekezi wananchi kulipa kodi mara mbili kwa matumizi ya miundombinu ya barabara.
“Ukizisoma sheria hizi kwa pamoja, mimi kama mkazi wa Kigamboni nikitumia daladala au gari binafsi, nalazimika kulipa kodi mara mbili kupitia kodi ya mafuta na tena tozo ya daraja. Hili ni kinyume na misingi ya usawa na haki kwa mujibu wa Katiba,” amesema Majaliwa.
Amesema yeye akiwa mwananchi wa kigamboni pamoja wananchi wa Kigamboni wamekuwa wakilazimika kulipa tozo h kila siku wanapovuka daraja hilo, jambo linalozidisha gharama za maisha na kuvunja misingi ya haki za kijamii na kiuchumi.
“Tunakwenda Mahakama Kuu kuomba itamke kwamba kitendo cha wananchi wa Kigamboni au mtu yeyote kulazimika kulipa tozo ya kuvuka daraja hilo ni kinyume cha Katiba,” amesema
Majaliwa amesema kuwa licha ya serikali kuzindua Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka 25, hakuna hatua zilizochukuliwa kupunguza au kuondoa tozo hiyo, akibainisha kuwa hali hiyo imeendelea kuwa kero kubwa kwa wakazi wa Kigamboni na wageni wanaotumia daraja hilo kila siku.
Ameongeza kuwa hatua ya kufungua kesi hiyo inalenga kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha haki ya usawa katika matumizi ya miundombinu ya umma inazingatiwa.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi