January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi wa Wilaya ya Kibaha watakiwa kutumia mvua zinazonyesha kupanda miti

Na Julieth Mkireri,KIBAHA

WAKAZI wa Wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia mvua zinazonyesha kupanda miti katika maeneo yao kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Wito huo umetolewa juzi katika shule ya Sekondari Picha ya ndege na Afisa Tarafa ya Kibaha Anatory Mhango wakati watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha wakipanda miti kuadhimisha miaka 60 ya uhuru.

Mhango ambaye alimwakilisha mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri katika shughuli hiyo ambayo ni endelevu alisema wakazi wa wilaya hiyo wanatakiwa kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kupata miti kuzunguka katika maeneo yao.

Alisema katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru Wilaya hiyo inatarajia kupanda miti 10,000 kwa ajili ya kutunza mazingira na pia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Mhango alizitaka shule nyingine kuiga mfano wa Sekondari ya Picha ya ndege kwa kupanda miti ya matunda na kivuli ambayo itawasaidia baadae.

Afisa Misitu wa Halmashauri ya mji wa Kibaha William Daudi alisema katika shule hiyo walipanda miti 200 ya matunda na kivuli katika maeneo yaliyoainishwa.

Aidha alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021-2022 Halmashauri ya Mji wa Kibaha inatarajia kupanda miti Zaidi ya 542,500 kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zilizopo ikiwemo wakala wa misitu (TFS).

Mwalimu wa Mazingira katika shule ya sekondari ya Picha ya Ndege Richard Ndunguru alisema katika shule yao yenye ukubwa wa ekari 11 tayari shule hiyo imeshapanda miti 1000 ikiwemo ya kivuli 980 na ya matunda 20.