December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi Msomera, Mkababu wavutiwa matumizi ya gesi, wampongeza Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraonlineHandeni

WAKAZI wa vijiji vya Msomera na Mkababu wilayani Handeni, Mkoani Tanga wameonesha kuridhishwa na ufanisi wa kampeni ya kumtua mama kuni kichwani iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu, kufuatia ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya gesi ya kupikia miongoni mwao badala ya mkaa na kuni kama ilivyokuwa ahapo awali.

Kwa mujibu wa wananchi hao, tangu kuanza kwa kampeni hiyo miezi mitatu iliyopita, wakazi hao hususani akina mama wamejikita zaidi katika matumizi ya gesi huku wakitaja changamoto kadhaa ikiwemo zile za kimazingira na kiafya zilizotokana na wao kutumia mkaa na kuni kama nishati za kupikia.

Wakizungumza walipotembelewa na viongozi kutoka wilaya ya Handeni, waliokuwa wakitathmini matumizi ya nishati safi katika wilaya hiyo, akina mama hao wamepongeza jitihada za Rais Dr. Samia Suluhu Hassan, za kuanzisha kampeni hiyo wakisema licha ya ugeni wake ,tayari imeonesha kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mwitikio chanya kutoka kwa wananchi hao.

“Mimi kwa mfano, huu ni mwezi wa tatu tangu nianze kutumia gesi, nimejiuliza maswali mengi sana na kujilaumu kwa nini nilichelewa kuanza kutumia gesi.

Kwa kweli nimepata manufaa mengi sana” Alisema Teresia Simon, mmoja wa wakaazi wa Kijiji cha Msomera na ambaye anatoka jamii ya Kimaasai.

Akina mama hao ni miongoni mwa wakaazi 1,500 walionufaika na mitungi ya gesi kutoka kwa kampuni ya Taifa Gas, katika mpango wa ushirikiano baina ya kampuni hiyo na Serikali kupitia Wizara ya Nishati , ambapo Taifa Gas imekabidhi Serikali mitungi 10,000 kwa ajili ya wananchi wake.

Mariam Khatib wa kata ya Chang’ombe amesema kwamba kinyume na alivyorajia, nishati ya gesi imempa mwamko mpya katika maisha yake kwa kuwa sasa anaweza kupika chakula chake kwa haraka hasa anapotayarisha chakula cha watoto ili waweze kuenda shuleni

Bi Teresia Simon, Mkazi wa Kijiji cha Msomela, Wilayani Handeni mkoani Tanga akiandaa chakula kwa kutumia nishati ya gesi ikiwa ni sehemu ya muitikio wa kampeni ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu iliyotambulishwa kijijini humo miezi mitatu iliyopita. Kwa mujibu wa wakazi wa Kijiji hicho, yangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya gesi ya kupikia miongoni mwao badala ya mkaa na kuni kama ilivyokuwa hapo awali.
Download all attachments as a zip file

“Sina tatizo la kuendelea kupambana na kuni tena ninapowashughulikia wanangu kuweza kula na kurudi shule. Gesi hii imenipa unafuu sana. Pia, nimejipamga kuhakikisha kwamba inapoisha, ninaijaza mara moja kwa sababu nimegundua ni nishati ambayo inaokoa muda na mambo mengi nyumbani na kuniruhusu kufanya kazi zingine” . Alisema Mariam Khatib.

Meneja wa programu hiyo ambaye pia ndio anasimamia Idara ya Mahusiano ya Umma katika kampuni ya Taifa Gas Bi. Angellah Bhoke aliesema fursa za kufungua maduka na vituo vya kujazia gesi katika program hiyo ilitolewa kwa baadhi ya wakaazi wa vijiji hivyo ili nao waweze kunufaika na fursa ya biashara kupitia mpango huo.

“Kila tunapotoa mitungi kwa umma, lazima pia tufungue maduka au vituo vya kujazia ili tuwape wepesi wananchi watakapohitaji kujaza. Kwa hivyo, Taifa Gas pia inatoa fursa za kibiashara kwa wakaazi kuweza kumiliki maduka au vituo vya kujaza gesi kama biashara zao wenyewe. Hii pia inasaidia katika kuinua maisha ya Watanzania”. Alisema Bi. Bhoke.

Tangu kuanzishwa kwa kampeni ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wadau wengi wa nishati safi wamejitokeza katika kupiga jeki kampeni hii. Taifa Gas kwa mfano imechangia zaidi ya mitungi 30,000, ambayo ni sawia na shillingi billioni 2 za kitanzania katika kuunga mkono kampeni hiyo.

Kwa upande wao, viongozi katika wilaya ya Handeni wametoa pongezi zao kwa kampeni hii ya Rais Samia na kusema kwamba wataendelea kuipigia chapuo hadi wananchi wote wa wilaya waweze kutumia nishati safi.

Bi Maria Lekipa Laitayok Mkazi wa Kitongoji wa Kitomgoji cha Mkababu, Wilayani Handeni mkoani Tanga akiandaa chakula kwa kutumia nishati ya gesi ikiwa ni sehemu ya muitikio wa kampeni ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu iliyotambulishwa kijijini humo miezi mitatu iliyopita. Kwa mujibu wa wakazi wa Kijiji hicho, yangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya gesi ya kupikia miongoni mwao badala ya mkaa na kuni kama ilivyokuwa hapo awali.

“Tuna imani kwamba ujio wa gesi hapa Handeni ni mwanzo mzuri kwetu na hatutarudi nyuma. Nimeagiza kupunguzwa kwa vibali vya ukataji wa miti inayotumika kuchoma mkaa kwa sababu sasa tuna lengo kuu la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa katika wilaya hii”. Napongeza Taifa Gas kwa ushirikiano huu ambao umetupendelea sisi wakaazi wa Handeni,” Alisema Mkuu wa wilaya ya Handeni, Albert Msando.