Na Suleiman Abeid, Times MajiraOnline, Shinyanga
WAKAZI wa Kata ya Didia katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamechanga kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ili kuwapunguzia watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda na kutoka shuleni.
Hatua ya wazazi hao inatokana na kata yao kutokuwa na shule ya sekondari iliyopo karibu hali iliyowalazimu watoto kutembea umbali wa kilometa nane kila siku kwenda kwenye shule ya Sekondari Didia iliyopo katika kijiji cha Bukumbi jirani na Makao Makuu ya kata hiyo.
Kutokana na maamuzi hayo ya wananchi Serikali kwa upande wake iliamua kuwashika mkono kwa kuwapatia fedha kiasi cha shilingi milioni 80 ambazo zimewezesha kwa kiasi kikubwa kukamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu 12 ya vyoo na tayari shule imeanza kazi ikiwa na wanafunzi wapatao 135.
Diwani wa kata ya Didia Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Richard Masele amesema kukamilika kwa sekondari hiyo ambayo imepewa jina la Sekondari ya Luhumbo mbali ya kuwapunguzia watoto kutembea umbali mrefu kwenda shuleni lakini pia imepunguza utoro na kuepusha vitendo vya ukatili walivyokuwa wakitendewa watoto wa kike.
“Kwa kifupi ujenzi wa Sekondari hii umewasaidia zaidi watoto wetu waliokuwa wakilazimika kutembea umbali mreru kila siku kwenda shuleni na kurudi nyumbani, umbali huu ulisababisha baadhi ya watoto kuwa na utoro wa rejareja maana wengi hawakuwa wakifika shuleni,”
“Lakini pia shule hii itapunguza kama siyo kukomesha kabisa matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wa kike walivyotendewa ikiwemo kubakwa ama kushawishiwa na vijizawadi, fedha au lifti za usafiri wa bodaboda na kujikuta wakibeba mimba katika umri mdogo na hivyo kukatisha masomo yao,” ameeleza diwani Masele.
Hata hivyo diwani huyo ameendelea kueleza kuwa pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa ikiwemo matundu 12 ya vyoo lakini bado shule inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa maabara na ofisi za walimu huku mipango ikiwa mbioni kujenga uzio kwenye shule hiyo mpya.
Diwani Masele ameendelea kueleza kwamba hamasa ya ujenzi wa shule hiyo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na kampeni ya kumpinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto inayoendeshwa na Klabu ya waandishi wa Habari Mkoani Shinyanga (SPC) ambapo wananchi wamehamasika na kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vya ukatili.
“Kutokana na kampeni hii inayoendeshwa na wadau wa kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wakishirikiana na waandishi wa habari habari chini ya ufadhili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WFT) jamii ilipokea mrejesho na kutenga ekari 10 kwa ajili ya ujenzi wa shule hii, tunaipongeza kampeni hii,” anaeleza Masele.
Ofisaelimu katika kata ya Didia, Justus Birago anasema tayari shule hiyo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa imeweza kupokea watoto 135 ambao wameanza masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa masomo na hivyo kuwaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kila siku.
“Hatuna budi kuwashukuru wadau wetu wa kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Halmashauri yetu ya wilaya ya Shinyanga pamoja na Serikali kwa hatua hii ya kuweza kupata shule mpya ya Sekondari ya Luhumbo, na sasa ni vyema tuwe pamoja katika ukamilishaji wa ofisi za walimu na maabara,”
“Naamini wananchi hasa wale wa maeneo ya kata hii ya Didia wameona nguvu ya vyombo vya habari katika suala zima la kupiga vita vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika halmashauri yetu, tukiendelea na ushirikiano huu wa awali ni wazi tutapiga hatua kubwa,” anaeleza Birago.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Juma Kisenha anasema hadi Februari 08, 2023 tayari wanafunzi 135 wameisharipoti shuleni na wanaendelea na masomo ambapo watoto wa kiume ni 74 na wasichana 61 huku akitoa wito kwa wazazi na wakazi wote wa kata ya Didia kuendelea kuchangia ili kukamilisha ujenzi wa vyumba vya ofisi na maabara.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo, Margareth Robert (13) na Petro Masunga wameishukuru Serikali kwa kukubali kuwaunga mkono wazazi wao kwa ajili ya kuanzisha shule mpya ambayo kwa upande wao imewaondolea kabisa adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kusoma kwenye shule ya sekondari ya Didia.
“Hatuna budi kuishukuru Serikali yetu ya awamu ya sita chini ya Rais Samia pamoja na wazazi wetu kwa kutujengea shule hii, kwa kweli imetuondolea kabisa ile adha ya kutembea kila siku umbali mrefu wa takribani kilometa nane kwenda na kutoka shuleni,”
“Kabla ya ujenzi wa shule hii baadhi ya wenzetu hasa wasichana walikuwa wakitendewa vitendo vya ukatili njiani wanapokwenda ama kutoka shuleni ambapo kama hawakubakwa basi walikutana na vishawishi mbalimbali kutoka kwa vijana wasio na tabia nzuri, sasa hali hii haitokuwepo tena,” anaeleza Petro Masunga.
More Stories
Mhagama atoa somo kwa watendaji
Ilemela nyama choma festival, yazinduliwa
Mchengerwa:Rufaa 5,589 za wagombea zimekubaliwa