Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amezindua rasmi chapa mpya za Yas na Mixx by Yas katika hafla iliyofanyika leo mkoani humo, huku akisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kurahisisha huduma za mawasiliano na fedha kwa njia ya kidijitali.
Uzinduzi huo ulizikutanisha taasisi za umma, sekta binafsi pamoja na mawakala wakubwa wa mawasiliano ili kupata uelewa wa mwelekeo mpya na maboresho yaliyoletwa na chapa hizo mpya, kufuatia mageuzi kutoka chapa ya awali ya Tigo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkude amesema teknolojia imeendelea kuwa injini ya maendeleo kwa Watanzania, ikitoa fursa mpya za kiuchumi, kijamii na kielimu kwa miongo kadhaa.

“Kupitia uzinduzi wa chapa hizi mbili, Yas na Mixx by Yas, tunashuhudia si tu mageuzi ya kimuonekano bali pia ya kimtazamo, mbinu na dira ya utoaji huduma bora zinazogusa maisha ya kila Mtanzania kwa namna ya kipekee,” amesema Mkude.
Aidha, ameeleza kuwa ujio wa chapa hizo unatoa suluhisho halisi kwa changamoto za mawasiliano na huduma za kifedha, jambo linaloendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora bila kujali mahali alipo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Yas – Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya amesema kwa zaidi ya miaka 30, chapa ya Tigo (ambayo sasa ni Yas) imekuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya kidijitali kwa kuwaunganisha Watanzania na kuwapatia fursa za kifedha kupitia teknolojia.
“Tunasonga mbele sasa na chapa mpya ya Yas. Yas si chapa tu bali ni falsafa ya mabadiliko, uvumbuzi na mshikamano wa kiuchumi,” amesema Mainoya.

Ameongeza kuwa, Yas inalenga kuwainua vijana, wafanyabiashara wadogo na wa kati, pamoja na kila Mtanzania anayesaka fursa ya kujikwamua kupitia teknolojia na huduma za kifedha za kisasa.
Uzinduzi huo ni hatua kubwa kwa sekta ya mawasiliano nchini, ukiashiria mwanzo wa sura mpya ya huduma zinazolenga kumgusa kila mwananchi kwa karibu zaidi.


More Stories
Chalamila:Dar ni salama,aelezea mafanikio na mipango ya maendeleo ya Mkoa
Ulaji vyakula vya aina moja,umri vyatajwa ongozeko la matatizo ya macho Mbeya
Kenya,Uganda zaanzisha mradi wa uendelezaji rasilimali za maji Angololo