Na Mwandishi wetu, Timesmajira-Dar
ZAIDI ya wananchi 200 wa Kata ya Buyuni, Jimbo la Ukonga,jijini Dar-es-Salaam, wamejitokeza katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo kushiriki zoezi la kupata Vitambulisho vya Taifa (NIDA), hatua inayolenga kuwawezesha kupata fursa mbalimbali ikiwemo mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo,mapema Januari 19,2026 Diwani wa Kata ya Buyuni, Jesca Msolla, amesema utoaji wa vitambulisho hivyo umetokana na maombi mengi kutoka kwa wananchi waliokuwa wakikosa fursa za mikopo kwa kukosa kitambulisho cha Taifa, hali iliyokuwa ikiwakwamisha kiuchumi.

Msolla amesema uamuzi wa kuleta huduma hiyo karibu na wananchi ulilenga kupunguza usumbufu na kuwasaidia wananchi wengi waliokuwa wakimfuata ofisini kuomba msaada wa kupata NIDA.
Amesema katika zoezi hilo mamlaka zote muhimu zimeshiriki ikiwemo NIDA, wanasheria pamoja na Idara ya Uhamiaji ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu Januari 19,2026,tumefanikisha uzinduzi wa huduma za NIDA katika Kata yetu ya Buyuni.Niliona kila fursa anayotaka mwananchi anaulizwa NIDA, hivyo nikaona ni vyema kutafuta fursa hii kwa manufaa ya wananchi wangu,” amesema Msolla.
Ameongeza kuwa kumekuwepo na fchangamoto ya baadhi ya wananchi kufika na nyaraka zisizokamilika, hali iliyosababisha kuendelea kutolewa elimu ili wananchi waweze kufahamu stahiki zinazohitajika.
Amefafanua kuwa zoezi hilo linawalenga wananchi ambao hawana kabisa vitambulisho vya NIDA, huku waliopoteza vitambulisho wakielekezwa kufuata taratibu katika ofisi kubwa za NIDA za kanda ya Ilala.
Kwa upande wake, Balozi wa zoezi hilo, Heri Shaban, amesema zoezi la utoaji wa vitambulisho vya Taifa lilianza Jimbo la Segerea kuanzia Januari 5 hadi 16, na leo Januari 19, 2026 limezinduliwa rasmi katika Jimbo la Ukonga likihusisha Kata za Buyuni na Chanika.
Amesema zoezi hilo linatarajiwa kufikia tamati Januari 30, 2026 ambapo
amewahimiza wananchi wa Jimbo la Ukonga, hususani Kata za Buyuni, Chanika, Zingiziwa na maeneo ya jirani, kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi walioshiriki zoezi hilo, akiwemo Mbaraka Kitonge na Mwidini Adam, wameipongeza Serikali pamoja na Diwani wa Kata ya Buyuni kwa kuwasogezea huduma ya vitambulisho vya Taifa karibu na maeneo yao, ambapo hatua hiyo itawarahisishia kupata fursa za kiuchumi na kijamii.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi