November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakazi 10,000 wanufaika na
ujenzi Zahanati Ramadhani

Na Mwandishi Wetu, Njombe,TimesmajiraOnline,Njombe

ZAHANATI ya Ramadhani iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Mtaa wa Ramadhani Kata ya Ramadhani Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe kwa gharama ya sh. milioni 103 imemaliza changamoto ya wananchi kukosa huduma za afya waliyokuwa wakikabiliana nayo kwa muda mrefu.

Tangu zanahati hiyo ianze kutoa huduma mwaka 2019 inahudumia wananchi 10,000 wa mtaa huo, huku idadi ya wagonjwa ikizidi kuongezeka wakiwemo wanaofika kuchukua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI

Hayo yamesemwa na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ramadhani, Dkt. Rehema Omary, wakati akieleza jinsi ujenzi wa zahanati hiyo iliyojengwa ulivyowezesha wananchi wa Mtaa Ramadhani kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya karibu na makazi yao.

Akithibitisha hilo, Dkt. Omary amesema kwa siku zahanati hiyo inahudumia wagonjwa 20 hadi 25 na kati ya hao asilimia 75 ya wagonjwa ni watoto na asilimia 25 na watu wazima.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ramadhani, Dkt. Rehema Omary

Amefafanua kwamba sehemu kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa na zahanati hiyo ni watoto na wazee ambao wapo kwenye kundi la msamaha wa matibabu.

Kwa mujibu wa Dkt. Omary Zahanati ya Ramadhani ilianza kutoa huduma mwaka 2019 na kwa sasa ina wafanyakazi wanne, daktari mmoja ambaye anahudumia vitengo vyote vikiwemo vya watoto, watu wazima, wajawazito na wanaohitaji upasuaji.

Aidha amesema zahanati hiyo ina muuguzi mmoja na medical attendant (wahudumu wa matibabu) wawili. Aidha amesema ina wataalam wasaidizi kwenye kazi mbalimbali ikiwemo kwa watu wanaenda kwenye zahanati hiyo kuchukua dawa za kufubaza virusi vya UKIMMWI.

Aidha, amesema zahanati hiyo ina Kliniki ya Huduma na Kinga (CTC) kwa upande wa wajawazito, huduma za uzazi wa mpango na vidonda

Amesema kwa mchanganuo wa huduma zinazotolewa kwenye zahanati hiyo, ni kieleleo kwamba uamuzi wa wananchi kuibua mradi huo na kisha TASAF kutoa fedha zilizofanikisha ujenzi wake ulikuwa sahihi, hasa kwa kuzingatia kwamba wananchi walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya maeneo mengine.

Dt. Omary amesema katika zahanati hiyo wanatoa huduma hadi saa 9.30 alasiri na baada ya hapo anabaki mfanyakazi mmoja kwa ajili ya kutoa huduma za dharara kwa wangonjwa wanaofika baada ya muda wa kazi.

Mwonekano wa nje wa Zahanati ya Ramadhani

Ameongeza kuwa ikishafika saa 12 anaondoka mhudumu wa zamu aliyekuwepo anaacha namba za simu kwenye ubao wa matangazo ili akitokea dharura wanapigiwa simu na wao wanafika na kuwasaidia kupata huduma.

Ili kuondokana na changamoto hiyo, Dkt. Omary amesema wananchi waliibua mradi wa nyumba ya watumishi na walipeleka maombi TASAF ambayo tayari imetoa fedha na ujenzi wa nyumba hiyo umeanza, hivyo baada ya kukamilika, watakuwa tayari kutoa huduma kwa wagonjwa kwa saa 24.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Ramadhani, Evaristo Mwimba, amesema mwaka 2017 kwenye mkutano mkuu waliibua mradi wa kutaka kujengewa zahanati kwa sababu eneo hilo halikuwahi kuwa na zahanati, huku likiwa na wakazi wasiopungua 10,000.

Amesema huduma nyingi walikuwa wakizipata kwenye kituo cha afya Mgewe, hivyo baada ya kuibua mradi huo walipeleka maombi yao kwa waratibu wa TASAF waliopo kwenye Halmashauri ya Mji Njombe ili waone namna ya kuwasaidia.

Mwaka 2018 zahanati hiyo ilianza kujengwa na mwaka 2019 ilianza kutumika, ambapo mbali na TASAF kujenga zahanati hiyo na wananchi walichangia asilimia sizizopongua 10 ya nguvu kazi. Pia anasema TASAF iliwapatia thamani za kutumia ndani ya zahanati hiyo.

“Kwa hiyo ile adha ya kupata huduma za afya haipo tena , naishukuru TASAF kwa kuzidi kutusaidia kwa sababu wametusaidia mradi mwingine wa ujenzi nyumba ya wafanyakazi wa zahanati hii na umeanza kutekelezwa.

Kupitia wananchi wa Ramadhani huduma zimesogezwa . Tunshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwani Serikali inatimiza wajibu wake kwa kutatua kero kubwa ambazo wananchi wanakuwa nazo na hilo linafanyika chini ya uongozi wa Samia, kero za afya zimetatuliwa na wananchi wanaendelea kupata huduma vizuri,” alisema.

Amesema kutokana na jinsi wananchi wa Mtaa wa Ramadhani walivyokuwa na uhitaji mkubwa wa zahanati hiyo na kwa sababu waliweka nguvu zao wakati wa ujenzi, wanatambua umuhimu wake, hivyo watakuwa sehemu ya walinzi wa miundombinu ya mradi huo.

Zahanati Ramadhani

Naye Joyce Ndendya (42) mkazi wa Mtaa wa Ramadhani amesema mradi huo umekuwa mkombozi mkubwa kwa akina mama na watoto, kwa sababu kipindi cha nyumba walikuwa wanapata shida kwa upande wa huduma ya mama na mtoto.

Anasema kabla ya hapo walikuwa wanapata huduma kituo cha afya Mgewe na sasa huduma ambazo walizokuwa wanazifuata huko wanazipata Ramadhani. Hata hivyo anaomba kwenye zahanati hiyo wapatiwe jengo maalum la kutoa huduma ya mama na mtoto, kwani licha ya huduma hiyo kuwepo kwenye zahanati hiyo,lakini wanahitaji jengo maalum.