Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
SERIKALI kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa mafunzo na kuwakabidhi majukumu wakaguzi wa ngozi 33,kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa,ili kuhakikisha ngozi inayozalishwa nchini inakuwa bora na yenye kiwango.
Hii ni kutokana na kati ya asilimia 100 ya ngozi zinazopelekwa kiwandani asilimia 10 ndizo zinafaa kusindikwa na kutengeneza bidhaa huku asilimia 90 hazifai kutokana na kukosa ubora unaotakiwa ambapo jambo hilo limekuwa likisababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara na wenye viwanda.
Akizungumza wakati wa ufungwaji wa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ngozi yaliyofanyika mkoani Mwanza,Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo,Usalama wa Chakula na Lishe,kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Gabriel Bura,amesema wakaguzi hao wa ngozi ni kutoka mikoa ya Mwanza,Shinyanga,Mara na Simiyu ambapo lengo la mafunzo hayo ni kuongeza usimamizi wa sheria ya biashara ya ngozi.
Pia kuhakikisha uzalishaji wa ngozi una kuwa bora kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda,kwani kumekuwa na changamoto ya ubora hafifu wa ngozi zinazozalishwa hapa nchini hasa kwenye maeneo ya machinjio,wakati wa usafirishaji na mfugaji mwenyewe.
Bura amesema,ii kukabiliana na changamoto hiyo Wizara imeona iteue na kuwakabidhi majukumu Wakaguzi hao waweze kusimamia ngozi kwenye machinjio wakati ngozi inazalishwa kwa kuhakikisha kwamba hazitobolewi, zinahifadhiwa vizuri kwa njia ile inayo kubalika ya kuwekea chumvi na zinapo safirishwa vibali vitolewe na zifike kwenye viwanda vilivyopo na vinavyofanya kazi ili kuepusha changamoto ya ngozi kutokufika kiwandani.
“Kuwepo kwa Wakaguzi kutasaidia kujua ngozi imetolewa lini na kwa kiasi gani na zinatarajiwa kufika wapi,ndio sababu ya mafunzo haya leo,na tunatarajia baada ya mafunzo haya ubora wa Ngozi utaongezeka mwanzo viwanda vilikuwa vinapata asilimia 10 tu ya ngozi Bora lakini tunaamini ubora wa ngozi utaongezeka kutoka asilimia 10 sasa hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2022, kuwa zikifika kiwandani zinaweza kusindikwa na kutengeneza bidhaa,” amesema Bura.
Sanjari na hayo amesema ubora wa ngozi unachangiwa na afya ya mnyama mwenyewe na kama ameathiriwa na magonjwa hata ngozi itakuwa haina ubora unaotakiwa kwaio kwa kutoa chanjo watakuwa wamedhibiti magonjwa ambapo kwa kumuogesha mnyama watakuwa wamesaidia asishambuliwe na wadudu mfano ng’ombe akiwa ameshambuliwa na kupe katika kusindika ngozi alama za kupe au michirizi itaonekana kwenye ile bidhaa itakayokuwa imezalishwa hivyo bidhaa hiyo haita uzwa kwa bei inayotakiwa.
Tayari kanuni ya chanjo imeisha elekeza bei ya kila chanjo kwa mnyama kwahiyo mfugaji atapata kwa bei ambayo ni elekezi.
Kwa upande wake Ofisa Ngozi Mstaafu Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Mkufunzi wa mafunzo hayo Emmanuel Muyinga amesema,moja ya maeneo ambayo amewasisitiza Wakaguzi wa Ngozi ni kusimamia wachunaji wa ngozi katika machinjio kwa sababu ndipo ngozi zinapozalishwa katika changamoto yote ya mnyororo wa thamani tatizo la uharibifu wa ngozi katika machinjio linachangia kwa kiwango kikubwa sana.
Muyinga amesema, ngozi ikisha tobolewa inapunguza thamani,hivyo amesisitiza namna ya kuhifadhi ngozi baada ya kuchuna ambapo ngozi inatakiwa isikae zaidi ya masaa manne katika machinjio baada ya kuchuna ili iweze kufika katika mkondo wa biashara na isioze.
Akifunga mafunzo hayo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmily Kasagala, amewahasa washiriki wa mafunzo hayo kujiepusha na vitendo vya ukosefu wa maadili na uonevu na badala yake wakajenge mazingira rafiki kwa wadau kufanya biashara kwa wepesi zaidi.
Kasagala amesema,mategemeo ya Serikali baada ya Wakaguzi wa Ngozi kupata mafunzo hayo ni kuwa watasimamia Sheria ya Biashara ya Ngozi na kanuni zake kwa weledi na uadilifu mkubwa, uzalishaji wa ngozi Bora kutoka kwenye machinjio na maghala,usindikaji na biashara ya zao la ngozi hasa tuhuma za utoroshaji wa ngozi nje ya nchi pamoja na kuhakikisha makusanyo yanayotokana na zao la ngozi yanaongezeka.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ,Mwenyekiti wa Maofisa Ngozi Kanda ya Ziwa Veran Mwaluko, amesema baada ya mafunzo hayo wametambua wanapaswa kukagua nini katika machinjio na kufanya nini katika kwenye maghala kwa hiyo wanaishukuru Wizara kwa kuwapatia mafunzo hayo huku akiwashauri wamiliki wa mifugo kuhakikisha wanapopeleka mifugo kwenye machinjio ngozi hazitobolewi ili kuondoa changamoto ya kuharibu ngozi na kupata vipande vivyokuwa na faida.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea