Na Daud Magesa, Timesmajira Online Mwanza
Wajawazito 100,wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, wamenufaika na msaada wa vifaa vya uzazi vyenye thamani ya milioni 5, vilivyotolewa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation.
Msaada huo unajumuisha ujenzi wa shimo la kisasa la kuhifadhi kondo la nyuma (placenta pit),Kituo cha Afya Makongoro,kilichopo Kata ya Mirongo lililogharimu milioni 5.4.Lengo likiwa ni kuboresha huduma za uzazi katika eneo hilo linalohudumia Wilaya tatu ikiwemo Sengerema na Misungwi.
Mwenyekiti wa taasisi ya The Desk & Chair Foundation, Alhaji Dk. Sibtain Meghjee,Septemba 25,2024, amesema taasisi hiyo imekamilisha ujenzi wa shimo hilo kwa ubora,na kukabidhi mradi huo kwa uongozi wa kituo hicho.
Amesema msaada huo unatolewa katika kipindi ambacho Waislamu duniani wanasherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), hivyo ni furaha kutoa vifaa hivyo muhimu kwa wajawazito.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makongoro, Dkt. Emma Maneno, ameleza kuwa ujenzi wa shimo hilo utaboresha usafi na mazingira katika kituo hicho, hasa katika huduma za afya ya uzazi, amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira safi kwa wahudumu na wagonjwa.
Amesema kituo hicho kinahudumia zaidi ya watu 25,000 kwa mwaka, kwa siku watu 250 hadi 300.Huku changamoto ni uhaba wa viti 30 (mabenchi) , kompyuta, vifaa vya matibabu, miundombinu ya umeme, umeme wa dharura na mashine ya alama za vidole (Biometric Scaner).
Diwani wa Kata ya Mirongo, Hamidu Seleman, amesema,msaada ilioyolewa na taasisi ya The Desk & Chair Foundation,unalenga kuboresha usalama wa akina mama na watoto.Hivyo amehimiza wadau kuendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za afya.
Kwa mujibu wa Diwani huyo, amesema Serikali imetenga milioni 500, kwa ajili ya uboreshaji wa huduma na miundombinu ya kituo hicho .
Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dkt. Furaha Mwakafwila, amesisitiza umuhimu wa kutumia vituo vya afya kwa ajili ya uzazi salama na kuhimiza akina mama kupeleka watoto kliniki kwa ajili ya chanjo.
Amesema atashangaa kuona wajawazito, wakiendelea kujifungulia nyumbani ama njiani ,ili hali serikali imeendelea kuboresha huduma , miundombinu,dawa na vifaa tiba,lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu.
Baadhi ya wajawazito akiwemo,Rebecca Chacha na Jacky Anthony,wamesema ,msaada huo utawasaidia kupunguza gharama za kujifungua na kuimarisha usalama wa watoto wao.
Awali Sheikh wa Bilal Muslimu Kanda Ziwa, Sheikh Hashimu Ramadhan,amesema”The Desk & Chair Foundation wanajitolea kuihudumia jamii kwa mahitaji yao,kazi iliyokuwa ikifanywa na Mtume, na ndio misaada hii kwa ajili ya wazazi wa kituo hiki cha afya,wanahitaji baraka na huruma akinamama ili kujifungua salama,”.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best