February 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waislamu Mwanza wapokea Ramadhani kwa maandamano ya kidini

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

WAUMINNI wa Dini ya Kiislamu wa Mkoa wa Mwanza Februari 22,2025,wameandamana (Zafa),kwa sherehe za kiimani kuupokea mwezi Mtukufu wa Ramadhani, wakiongozwa na Sheikh Hassan Kabeke.

Zafa hiyo ilijumuisha waumini kutoka maeneo mbalimbali ya jiji, na yalianza kutoka Msikiti wa Raudhwa uliopo Mtaa wa Lumumba, yakipitia barabara kuu za Nyerere, Nkurumah, Uhuru, Makongoro, Kenyatta na Posta kabla ya kufika Uwanja wa Nyamagana, ambapo walipokelewa na Sheikh Haruna Kichwabuta, ambaye ni Mwenyekiti wa Masheikh Tanzania na Sheikh wa Mkoa wa Kagera.

Sheikh Kichwabuta akizungumza baada ya kupokea Zafa hiyo amehimiza umuhimu wa kuukaribisha mwezi wa Ramadhani kwa imani thabiti, akifafanua kwamba ni mwezi bora kuliko miezi mingine, ambapo Qur’ani ilishushwa na milango ya pepo hufunguliwa.

Amesma Zafa hiyo  ya kidini ni sehemu ya sherehe za kiimani zinazofanyika kila mwaka ili kuukaribisha mwezi wa Ramadhani,ambapo kipindi hicho ni cha kufanya ibada na kujitakasa.

Ambapo waumini wa Kiislamu wanatambua Ramadhani ni mwezi wa baraka na msamaha, na maadhimisho haya yanatoa fursa ya kuimarisha imani na kushirikiana kama jamii ya kiroho,hivyo ni muhimu katika maisha ya kila Muislamu kujitafakari na kufanya ibada kwa wingi.

“Ninawashukuru Jumuiya ya kuendeleza Qu’ran na Sunna(JUQUSUTA) ya Mtume Muhammad S.A.W ambao ni wasimamizi wa Maulid  katika taifa hili. Zafa hii si ya kwanza, ilianzia Madina na tunajitahidi kumhudhurisha Mtume,”amesema.

Pia amewakumbusha waumini hao umuhimu wa umoja na mshikamano katika kipindi hiki huku akiwahimiza waumini kukusanyika usiku kwa ajili ya kujifunza na kuelewa mambo muhimu yanayotarajiwa kufanyika nchini, ikiwa ni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Kauli mbiu yetu ni kuna maisha baada ya uchaguzi; linda amani, chagua kwa hekima,tufanye juhudi za kuhakikisha kuwa tunaishi kwa amani na utulivu, ili kuleta maendeleo ya kweli,” amesema.