December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waiomba serikali kutenga bajeti ya mfumo wa elimu jumuishi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Licha ya jitihada za serikali za kuboresha mazingira rafiki ya utoaji elimu jumuishi na ustawi wa watoto, imeelezwa kuwa uhaba wa miundombinu rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu shuleni umekuwa kikwazo.

Hivyo wito umetolewa kwa serikali kuweka kipaumbele na kutenga bajeti juu ya mfumo wa elimu jumuishi ikihusisha vifaa, miundombinu na wataalamu.

Hayo yameelezwa Juni 16,mwaka huu na Josephine Bakita wakati akisoma risala kwa niaba ya watoto wa Mkoa wa Mwanza katika siku ya maadhimisho ya Mtoto wa Afrika kimkoa yaliofanyika jijini hapa ambayo uadhimishwa kila ifikapo Juni 16,ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo”Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa,maadili na stadi za kazi”.

Josephine ameeleza kuwa serikali imefanikiwa kujenga shule nyingi nchini na kuweka mfumo wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo watoto wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu wanaipata elimu sawa.

“Pamoja na jitihada hizo bado kuna changamoto zinazotukabili sisi watoto wa Mkoa wa Mwanza ikiwemo shule nyingi hazina miundombinu rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu ikijumuisha ukosefu wa njia za magurudumu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa viungo wanaotumia viti mwendo,” ameeleza Josephine.

Pia ameeleza changamoto nyingine ni uhaba wa vyoo vinavyofaa kwa watoto wenye ulemavu pamoja na mabweni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwani wengi hulazimika kuishi nyumbani na kutumia muda mrefu kwenda kupata elimu shuleni na kurudi nyumbani.

Shule zina upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunza vinavyofaa kwa watoto wenye mahitaji maalumu kama vile vitabu vya nukta nundu,vifaa saidizi vya usikivu(shime sikio) na viti mwendo kwa ajili ya wenye ulemavu wa viungo.

Huku shule zikiwa hazina walimu wa kutosha hii ina maana kuwa walimu wengi hawana ujuzi unaohitajika kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu.

“Serikali na wadau kuungana katika kuboresha miundombinu rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu na kujenga shule zenye mazingira jumuishi hasa kwa maeneo ya vijijini huku vyombo vya habari vikihamasisha kuhusu umuhimu wa elimu jumuishi,”amesema Josephine.

Naye mtoto mwingine Brigita Edward ametoa wito kwa serikali na wadau wa elimu kujitolea rasilimali na utaalamu wa elimu ili kuweka sera na programu zinazozingatia mazingira maalumu na wezeshi ya kupata elimu.

“Mazingira yatakayosaidia ulinzi wa wasichana na wavulana,watoto wenye ulemavu,vijana ,watoto wasio na wazazi au walezi,manusura wa ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kijinsia na kingono,vitendo vya madhara na watoto wengi walio katika hatari kwani elimu ndiyo fursa pekee ya kupata maisha bora ya baadae,”.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda katika maadhimisho hayo amesema kuwa serikali mkoani humo imekuwa ikishirikiana na wadau kuhakikisha vifaa saidizi kwa watoto wenye mahitaji maalumu vinapatikana huku akisisitiza kuwa kama kuna mtoto mwenye uhitaji wa kiti mwendo basi afike ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupata kifaa hicho

“Changamoto ambazo mmezieleza tumezichukua tutazifanyia kazi lakini nyingine zimeisha anza kufanyiwa kazi mfano suala la walimu wa wanafunzi wa mahitaji maalumu sasa hivi serikali kila inapoajiri watumishi hususani walimu lazima ina ajiri walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu,”ameeleza Elikana na kuongeza kuwa

“Pia tuna shule za mahitaji maalumu ambazo zimejengwa kwa kidato cha kwanza ikiwemo shule ya sekondari ya wavulana Bwiru inachukua wanafunzi hao na serikali imeendelea kuboresha kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wenye mahitaji maalumu wanapokelewa,tuna shule maalumu ya wasichana ya Mwanza(Mwanza Girls) iliopo wilayani Magu inachukua pia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwaio serikali inafanyia kazi na itaendelea kufanyia kazi hizi changamoto zilizobainishwa,”.

Meneja wa Ushawishi,Utetezi na Mawasiliano kutoka shirika la Plan International Secilia Bosco,amaleeza kuwa shirika hilo katika suala zima la elimu jumuishi wanahakikisha katika miradi yao yote wanayoifanya ya maendeleo wanakuwa na jicho la pekee la kuangalia mahitaji maalumu ya watoto.

“Katika shule ambazo tunafanya kazi tunahakikisha kwamba kwanza kuna kuwa na miundombinu rafiki kwa watoto hao wenye mahitaji maalumu,tunathamini sana watoto wote na hivyo tunatilia mkazo kwenye ujumuishi siyo tu kwa wenye ulemavu wa viungo lakini pia ata wale wenye mahitaji maalumu ya kisaikolojia,kiakili na kuna ulemavu ambao hauonekani kama nchi tunapaswa kuzingatia na kujifunza pia,”.

Secilia ameeleza kuwa katika maadhimisho hayo wameweza kuwakutanisha watoto wa Mkoa wa Mwanza takribani 300 ili waweze kupaza sauti zao ili wadau wa masuala ya watoto wazisikie .

“Kama wadau tunajua vitendo vya ukatili ni vingi na Mwanza ni kati ya Mikoa ambayo ina kesi nyingi za ukatili ambapo kupitia maadhimisho haya watoto wamekuwa na uelewa kuhusiana na ukatili na wanajua namna gani ya kutoa taarifa,”amesema Secilia.

Ofisa Elimu,Elimu Maalum Awali na Msingi Jiji la Mwanza,Zakiah Ahmed,ameeleza kama Mkoa wa Mwanza unatekeleza kauli mbiu ya maadhimisho hayo ambapo watoto wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu wanapewa elimu sawa kwa kuzingatia mahitaji yao,uelewa wao na uwezo wao pia.

“Sasa hivi tunaletewa miradi mbalimbali kwa shule za msingi na sekondari na vipaumbele vinatolewa kwa madarasa yazingatie umuhimu wa mtoto mwenye mahitaji maalumu,kmkila mradi wa vyoo lazima izingatie kuwa na choo cha mwanafunzi mwenyewe mahitaji maalumu,”

Amesema Halmashauri ya Jiji la Mwanza ina zaidi ya shule jumuishi 43 na vitengo vinavyotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu zaidi ya 14 hiyo inaonesha wanavyotekeleza kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo”elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi”.

Huku akitolea mfano mtoto mwenye ulemavu wa akili atafundishwa namna ya kujitegemea yeye hivyo kuleta chachu kwa familia,jamii na taifa hivyo kwa sasa serikali inatekeleza kauli mbiu hiyo.

“Mkakati wa ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum ndio msingi wa kusaidia wadau wa elimu kuweza kuwaibua na kuwapa shule na kuwaweka katika sehemu zinazostahili wito kwa wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalumu wasiwafiche watoto wao ili wadau waweze kuwafikia na kufahamu changamoto zao,”.