Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mwanza
Ili kutatua changamoto ya ukosefu wa wa taulo za kike shuleni, walimu na wanafunzi katika shule za sekondari Kayenze na Sangabuye zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kujenga chumba kitakachotumika kama benki ya kuhifadhia vifaa hivyo vya kujisitiri wasichana wawapo shuleni wakati wa hedhi.
Ambapo kupitia benki hiyo wadau,jamii na watu mbalimbali wataweza kuchangia huku wakiomba serikali na wadau kuangalia suala la taulo za kike kwa jicho la tatu hili zipatikane wakati wote shuleni kwa sababu ni hitaji la msingi kwa watoto wa kike.
Ombi hilo limetolewa Juni 4,2024 mara baada ya baadhi ya waandishi wa habari na wadau wengine kutembelea shule hizo kwa ajili ya kuwapatia taulo za kike zilizotolewa na Taasisi ya Desk and Chair Foundation, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Eagle Entertainment,Peter Temu na Mohamed Seif ambapo takribani wanafunzi 350 wamefikiwa.
Mwalimu wa shule ya sekondari Sangabuye Elizabeth Richard, ameeleza kuwa katika shule hiyo wana watoto wa kike zaidi ya 400 huku upatikanaji wa vifaa vya kujistiri wakati wa hedhi kwa wanafunzi hao ni changamoto kwa sababu wengi wao wanatokea familia zenye mazingira magumu.
“Tukipata hivi vifaa na kuwafikia moja kwa moja watoto wenye uhitaji maana ata ujaji wa shule’mahudhurio’ utakuwa mkubwa na pia watakuwa katika mazingira salama ya kuweza kusoma hivyo tunaomba wadau mbalimbali waweze kujitokeza kusaidia watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao,”amesema Mwalimu Elizabeth.
Pia Mwalimu Elizabeth ameiomba serikali kuangalia kwa jicho jingine suala la upatikanaji wa taulo za kike nchini kwa sababu wanafunzi hao ndio wa mama wa kesho “kwani wasipo wajali sasa maisha yajayo hatutakuwa na taifa zuri ukimsaidia mtoto wa kike unakuwa umesaidia taifa”.
Serikali iwafikie watoto wa kike kwa kuweza kujenga benki ya pedi shuleni maana zikiwepo kwa wingi ni rahisi kuwafikia na kuondokana na changamoto hiyo ambayo wakati mwingine inawafanya washindwe kuhudhuria masomo kwa siku kadhaa.
Mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Sangabuye Jesca Alfred amelishukuru kwa Shirika la Desk and chair Foundation na wadau wengine kupitia waandishi wa habari kwa kuwapatia taulo za kike ili waweze kutimiza ndoto zao.
“Kwani kuna baadhi ya wasichana wanashindwa kuhudhuria masomo kwa sababu ya kukosa taulo za kike ‘ped’ kwa ajili ya kujihifadhia wakati wakiwa hedhini,tunaomba wadau waendelee kutufadhili kwa kutupatia vifaa hivyo ili tuweze kuhudhuria masomo wakati wote na tufaulu mitihani bila hofu,” ameeleza Jesca.
Pia Jesca ameeleza kuwa vifaa vingine wanavyovitumia kwa ajili ya kujistiri mbadala na pedi ni vitambaa kama vile leso na wakati mwingine wanaenda kwa fundi nguo wanamwambia awashonee vitambaa.
Naye Amina Haruna kutoka shule ya sekondari Sangabuye ameeleza kuwa mzazi anapomnyima fedha kwa ajili ya kununua taulo za kike anaweza kusababisha mtoto huyo kujiingizia katika mambo hatari ili aweze kupata kifaa hicho kwa ajili ya kujistiri ikiwemo kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi katika umri mdogo.
“Pedi mlizotupa leo mmetusaidia na kutuepusha kwenye hatari ya kujiingiza katika mapenzi,tunawaomba wazazi watuwezeshe pedi kwani tukiwa shule na hatuna vifaa vya kujistiri kusema ukweli ata kwangu mimi uwa najiona kuwa sijiamini na kuwa sipo huru kujifunza Mwalimu anaweza kuwa anafundisha mimi mawazo hayapo kwenye kile kinachofundishwa ila naweza je nikiamka nikiwa nimechafuka itakuwaje,”ameeleza Amina na kuongeza kuwa;
“Vitu vingine ambavyo uwa tunatumia ni vitambaa hususani vile vya kufungia watoto’vidaso’ mara nyingine ndio tunapenda kutumia tusipokuwa na taulo za kike,”.
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze Vannesa Elias,ameiomba serikali kupunguza bei ya taulo za kike kwani ni kubwa ukilinganisha na uwezo wa familia ambazo nyingi ni duni haziwezi kumudu gharama ya vifaa hivyo.
Happiness Mfaume mwanafunzi wa shule ya sekondari Kayenze,ameeleza kuwa msaada huo wa pedi utawasaidia kuepuka vishawishi na kupunguza gharama kwa wazazi kwani wanatoka mazingira tofauti kuna wengine hawezi kumudu gharama hivyo ufadhili huo unawafanya wawe kitu kimoja na kufikia malengo pamoja.
Kwa upande wake Mwandishi wa Habari wa Majira Judith Ferdinand,amewaomba wadau wengine kuendelea kuiunga mkono serikali kwa kuhakikisha wanawasaidia watoto wa kike kuhudhuria masomo nyakati zote kulingana na ratiba ya masomo iliowekwa na serikali kwa kuchangia taulo za kike shuleni ili zipatikane wakati wote.
“Tumetembelea shule ya sekondari Sangabuye na Kayenze tukiwa tumeungana waandishi wa habari pamoja na wadau wengine kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi wa kike taulo za kike,tumefanya hivyo kupitia kauli mbiu yetu ya Tuwavishe watimize ndoto zao,matamanio yetu ni kuona watoto wa kike wanapokuwa shuleni hawakutani na changamoto ya ukosefu wa taulo za kike huku shule zote za msingi na sekondari kunakuwa na benki ya taulo za kike ambayo itasaidia hupatikanaji wa vifaa hivyo wakati wote,”.
More Stories
Rais Samia amlilia Dkt. Ndugulile
Makada wa CHADEMA,mbaroni kwa tuhuma za kukimbia na karatasi za kuraÂ
Rais Samia afanya uteuzi wa viongozi mbalimbali