November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waiomba MWAUWASA kuboresha huduma ya maji

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wananchi wa Mlima Rada uliopo Kata ya Kiseke wilayani Ilemela mkoani Mwanza wameiomba serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA), iendelee kuboresha huduma ya maji ili yaweze kuwafikia wote kwa usawa na kupunguza mgao uliopo.

Ombi hilo wamelitoa kwa nyakati tofauti Julai 26,2024 mara baada ya Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew,kutembelea makazi yao kwa ajili ya kuhakikisha kama huduma ya maji inawafikia wananchi pamoja kubaini changamoto zilizopo.

Mmoja wa wananchi wa Mlima Rada Rehema Petro, akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Maji, ameeleza kuwa maji wanapata kwa wiki mara tatu hadi nne inategemea na wakati.

Amesema awali maji walikuwa wanatoa kwenye mabomba mbali na makazi yao na yasipo kuwepo walilazimika kuyafuata mbali kwenye visima.

“Hali ya sasa hivi ya upatikanaji wa maji katika maeneo yetu ni afadhali huwezi kulinganisha na zamani,tulikuwa tunatoa maji mbali kiasi kwamba ndoo moja kuifikisha nyumbani kifua kilikuwa kimebana,”ameeleza Rehema na kuongeza kuwa

“Nilikuwa naathirika sana unatoka saa kumi na moja alfajili kufuata maji,unarudi hapa saa mbili,saa tatu unakuta watoto wameisha pigwa njaa ya uhakika,naiomba serikali iongeze huduma hiyo ya maji kwa kasi zaidi kwani maji ni uhai,”.

Hassan Kweza,amesema kwa sasa angalau hawawezi kumaliza siku mbili bila maji kutoka na kwa wiki hizi tatu zilizopita wamekuwa wanapata maji kwa wingi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tenki la maji Buswelu.

“Awali tulikuwa tunafuata maji mbali tena kwa foleni na wakati mwingine unashinda njaa,naiomba serikali kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji zile itilafu ndogo ndogo ili tupate maji wote kwa usawa,”.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew, ameeleza kuwa maji yanatakiwa kupatikana kwa siku tano ,ratiba na miundombinu ya maji inatakiwa kuangaliwa upya ili kuweza kuleta usawa wa hupatikanaji wa huduma hiyo.

Sanjari na hayo Mhandisi Kundo amewataka wananchi wanao uza maji kwa wengine ndoo ya lita 20 bei isizidi sh.50 huku akiitaka MWAUWASA kubaini wanazouza maji na kuwafungia dira za maji za lipa kadri unavyotumia(Luku Meter).