January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Picha ya mtandao

Wahudumu wa baa watakiwa wavae barakoa

Na Eliasa Ally, Iringa

MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ameagiza wamiliki wa baa kuhakikisha wafanyakazi wao wanavaa barakoa kwa ajili ya kujikinga na virusi vya corona (COVID-19).

Pia amemtaka kila mmiliki wa sehemu zenye mikusanyiko ya watu kuhakikisha kuna maji yanayotiririka na sabuni kwa ajili ya watu kunawa.

Akizungumza na wamiliki wa baa, Mkuu huyo wa wilaya alisema ni muhimu wahudumu hao kuhakikisha wananawa mikono ikiwemo kutumia vitakasa mikono.

Aidha, alisema wilaya hiyo imejipanga vyema na iwapo itatokea mtu mwenye maambukizi hatua zitachukuliwa za kumtenga na kuwachukua na kuwatenga na jamii.

Kwa mujibu wa Kasesela, wamiliki hao wanapaswa kuhakikisha wateja na wahudumu wanakaa umbali uliopendekezwa na wizara ikiwa ni hatua ya kujikinga na maambukizi.

ìWale wote wanaokuwa kwenye maeneo ya burudani wanapaswa kukaa kwa umbali unaotakiwa na watakaokiuka watachukuliwa hatua kwa kufunga biashara zao,îalisema.

Aidha, kwa kuonyesha mfano, Mkuu huyo wa wilaya ambaye alikuwa amevaa barakoa, alisema ni lazima watu kukaa kwa umbali wa mita moja, ikiwemo wapenzi kuhakikisha wanajitenga.

Kuhusu muda wa kufunga baa, Kasesela alisema manispaa hiyo itaangalia muda wa kufunga kwa kuwa wapo wanaoendelea kufanya biashara hadi usiku wa manane.

Aidha, alisema anakusudia kukutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara mkoani humo kujadili suala hilo kwa kina.