Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Watoa huduma za afya ngazi ya jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza wamepatiwa mafunzo kazini ya lishe bora na umuhimu wa vitamini A na dawa za minyoo kwa watoto wa chini ya miaka mitano.
Hii ikiwa ni njia ya kutambua umuhimu wa lishe kwa mama na mtoto ambayo kimsingi husaidia kukua vyema kwa mtoto kimwili kuwa na kinga pamoja na nguvu za kupambana na magonjwa hivyo kuharakisha ukuaji wake.

Mafunzo hayo yametolewa Desemba 11,2025, na Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Pili Kassim,ambapo amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na kuongeza ufanisi kwa watoa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili waweze kufanya kazi katika mitaa yao.
“Pia kuhakikisha huduma za lishe zinafanya vizuri na tunategemea baada ya mafunzo haya huduma za kilishe zitaimarika katika vituo vyetu vya kutolea huduma,” amesema Pili.
Kwa upande mtoa huduma za afya ngazi ya jamii kutokea Kata ya Kahama,Lukona Nangulo,amesema mafunzo hayo yamemumwezesha kutumia kipimo cha utepe (muaki), kupima uzito kwa ajili ya kutambua hali ya afya ya mtoto.
“Nitafanyia kazi mafunzo niliyopatiwa leo kwa kuwapima watoto ili kutambua wenye udumavu na wasiokuwa na udumavu, na wale watakaokutwa na udumavu nitawashauri mama zao kuwaandalia chakula cha lishe na watakao endelea kuwa na hali hiyo wapelekwe kituo cha afya,”amesema Lukona.

Naye mhudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka Kata ya Kayenze,. Angelina Sulyu,amesema kupitia mafunzo hayo yamewaongezea ufahamu kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu lishe bora kwa mtoto.
Hivyo amewashauri wakina mama kutokuwafungia watoto wao ndani bali wawapeleke kwenye vituo vya afya ili waweze kupata huduma na elimu mbalimbali zinazohusu lishe.


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama