Na Bakari Lulela,Timesmajira. Online
WANAFUNZI wanaohitimu mafunzo ya kozi mbalimbali katika Chuo cha Amana Vijana Centre, wametakiwa kutumia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri za wilaya, ili kuendeleza mipango endelevu ya kujipatia kipato.
Akizungumza jijini Dar esalaam Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Nassoro wakati wa mahafali ya 12 ya Chuo cha Amana Vijana Centre, ambapo amewataka kuacha kutegemea kuajiriwa pekee bali watumie fursa ya mikopo hiyo ili waweze kujiajiri.
“Nimesikia changamoto zenu kwenye risala, mmetaja kwamba eneo lililopo kwa sasa ni finyu, nitakutana na Mkuu wa wilaya nimuelezee, ndugu zangu kuna wadau wengi tu ambao tukifanya harambee watatusaidia kwa hiyo nawaahidi hili nitalifikisha sehemu sahihi na tutapanga lini tufanye hii harambee,” amesema.
Nassoro ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto zinazokikumba chuo hicho, atatafuta wadau mbalimbali na kufanya harambee ya kuchangia fedha zitakazotumika kuboresha miundombinu ya chuo hicho.
Naye Mkurugenzi wa chuo hicho, Philipo Ndokeji amesema chuo chake kinasawasaida vijana kufikia malengo yao kwa kuwapatia ujuzi na maarifa kwa lengo la kuendeleza maisha yao ama kusaidia familia zao kuodokana na ukali wa maisha.
Mkurugenzi huyo amesema jumla ya wahitimu wa kozi mbalimbali 160, walipatiwa vyeti vyao ikiwemo wahitimu wa kozi za udereva, upambaji, hotelia, kompyuta, ufundi cherehani na saluni.
Hata hivyo, Ndokeji amesema kuwa chuo chake kitaendelea kutoa elimu bora itakayowawezesha vijana kukabiliana na ushindani wa soko la ajira na vijana wengi waliopitia chuoni hapo, wamekuwa wakifanya vizuri katika taasisi na makampuni mbalimbali.
Kwa upande wake Katibu wa Taasisi ya Wakati Wako ni Sasa ambayo inaendeleza vipaji vya kuimba na kucheza kwa vijana na kusaidia watu wenye uhitaji nchini, Hassan Ally amewataka wahitimu hao kuwa na nidhamu kazini pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kufanikiwa katika kazi zao.
Baadhi ya wahitimu hao akiwemo Jonh Joviti (hotelia) na Fatuma (kompyuta), kwa nyakati tofauti wamesema watazingatia yale waliyoelekezwa na elimu waliyoipata itawasaidia kuajiriwa au kujiajiri, ili waweze kupata maendeleo yao na kusaidia familia zao.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best