Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,wamehimizwa kuzifahamu sheria za ardhi kwani wawekezaji wengi wanakwenda kutafuta ardhi katika maeneo yao kwa lengo la kuwekeza.
Hayo yamesemwa Leo na Kaimu Mkuu wa wilya ya Nkasi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga,Nyakia Chirukie,kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Madiwani ambapo amesisitiza umuhimu wa madiwani hao kuzifahamu walau sheria za awali kuhusu ardhi.

Amesema kuwa ardhi ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo kwa jamii, ni vizuri ikasimamiwa vyema kwa kufuata misingi ya kisheria ili kuondoa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza na kuleta mifarakano katika jamii.
Hivyo amewasihi mafunzo hayo yakawajenge na kutambua misingi ya kazi na mipaka yao ili kuondoa migongano ya kiuongozi katika maeneo yao wanayoyaongoza.
Pia amewataka Madiwani hao kuongeza kasi ya kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kwa wote lakini kuhakikisha mpango wa kuwapatia bima bure kaya masikini unafanikiwa.
Kwani kasi ya watu wanaotoka kaya masikini kujiunga na mfuko huo ni ndogo,hivyo Madiwani wahakikishe wananchi waliotambuliwa kupitia TASAF wanajitokeza na kujiandikisha ili weweze kunufaika na mpango huo wa bima ya afya kwa wote.
Amefafanua kuwa zoezi la kuziandikisha kaya masikini na kupewa bima ya afya bure lilipasea kukamilika Februari 2,2026.Baada ya kuona zoezi hilo linasuasua wameongeza siku hadi Machi 22,2026 mwaka huu.
Ambapo amesema kwa Wilaya ya Nkasi wanufaika wa mfuko huo waliojitokeza hadi sasa ni 3,608 sawa na asilimia 10 pekee hivyo Madiwani wanalo jukumu la kutoa hamasa kwa wananchi wao ili waweze kujitokeza kupata bima hizo za afya.
Diwani wa Kata ya Majengo Shida Sinkala, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kufahamu mipaka yao na namna bora ya kuwatumikia wananchi.

Madiwani hao wamepewa mafunzo mbalimbali ikiwemo masuala ya uongozi na utawala,sheria za uendeshaji wa shughuli za Serikali za mitaa,muundo,majukumu na madaraka ya serikali za mitaa,uendeshaji wa vikao na mikutano katika mamlaka za serikali za mitaa,mipango,bajeti na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Pamoja na usimamizi na udhibiti wa fedha katika mamlaka ya serikali za mitaa,usimamizi wa watumishi katika mamlaka za serikali za mitaa,usimamizi wa ardhi na wajibu ,majukumu,haki na stahiki za Diwani.


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama