March 31, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahimizwa kutumia taa za nishati ya jua badala ya vibatari

*Sun King yatoa ajira zaidi ya 3000 kwa vijana nchini

*Yasisitiza kuunga mkono matumizi ya nishati safi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wananchi wa Kata ya Bukandwe wilayani Magu mkoani Mwanza,wamehimizwa kuacha na matumizi ya vibatari na badala yake watumie taa zinazotumia nishati ya jua(solar).

Wito huo umetolewa Machi 28,2025 na Ofisa Tarafa wa Tarafa ya Sanjo wilayani Magu,Pepertua John kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo,wakati wa ufunguzi wa duka la Sun King, stendi ya Isangijo Kata Bukandwe wilayani humo ambalo ni la nne kwa Mkoa wa Mwanza.

Pepertua amesema,matumizi ya vibatari yanasababisha watu kuugua macho na vifua kutokana na moshi unaotoka,hivyo wakitumia taa zinazotumia nishati ya jua ikiwemo za kampuni hiyo ya Sun King, itasaidia kuondokana na magonjwa hayo, wanafunzi kusoma pamoja na wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa uhakika wakati wa usiku.

“Hii ni fursa kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa na nishati ya umeme wa Tanesco,kutumia taa hizo hususani baadhi ya vijiji wilayani humu ambavyo bado Serikali haijavifikishia huduma hiyo,”amesema Pepertua.

Msimamizi wa Biashara nchini Tanzania wa kampuni ya Sun King, Juma Mohamed,amesema kwa sasa kampuni hiyo imejikita kuuza taa zinazotumia nishati ya jua ili kuwasaidia wananchi kuondokana na matumizi ya nishati chafu ikiwemo vibatari vinavyotumia mafuta,hivyo wamefungua duka hilo ili kusogeza huduma kwa wananchi ambapo kwa sasa wana maduka 65 na wanatarajia zaidi ya hayo mwakani.

Mohamed amesema, kampuni hiyo pia inaunga mkono mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuleta nishati mbadala ili kupunguza au kuzuia uzalishaji wa hewa ukaa ambayo inachangia kuharibu mazingira.

“Tupo mstari wa mbele kuhakikisha tunaunga mkono ajenda ya kidunia na Tanzania ni mudau namba moja ya kuhakikisha hewa ukaa inapungua duniani.Pia tunatekeleza ajenda ya Serikali ya kukuza uchumi wa wananchi kwa kutoa ajira kwa vijana wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika na wenye elimu zaidi ambao wamebadilisha maisha yao kwa kiasi kikubwa,”.

Kwa upande wake Balozi wa kampuni ya Sun King, Mrisho Mpoto maarufu Mjomba, amesema wameonesha wananchi madhara ya matumizi ya nishati isiyo safi na faida za nishati safi huku akisisitiza kuwa licha ya kampuni hiyo kuunga mkono suala la matumizi ya nishati safi pia imetoa ajira kwa vijana zaidi ya 3,000 nchi nzima na ni fursa zaidi kwa vijana wengine kupata ajira na kuweza kujikwamua kiuchumi.

“Lengo ni kuhamasisha watu kutoka katika matumizi ya nishati chafu hadi nishati safi,na kinara ni Rais Samia Suluhu Hassan ambaye mwenye lengo la kufikia mwaka 2034,asilimia 80 wawe wanatumia nishati safi na kufanikisha hilo ushiriki wa kampuni binafsi kama hiyo ya Sun King ni muhimu,”.