*Ni wale ambao walikisa fursa ya kusoma katika mfumo rasmi wa elimu
Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online -Rukwa
Wito umetolewa kwa wananchi ambao hawakufanikiwa kupata elimu ya mfumo rasmi kuchangamkia fursa ya elimu ya Watu Wazima inayotolewa nchini kote bila kujali umri wao na aibu, kwani upo utaratibu nzuri wa wao kufundishwa.
Hayo yamebainishwa Septemba 2, 2025, na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi katika sherehe za kilele cha maadhimisho ya wiki ya Elimu ya Watu Wazima,Peter Lijualikali, zilizofanyika yaliofanyika chuo cha VETA Paramawe mkoani Rukwa ,huku akitoa wito kwa watu wote kuishika elimu na kuipigania.

Awali Ofisa Elimu ya Watu Wazima sekondari na elimu nje ya mfumo rasmi,Thomas Mhagama kwa niaba ya Ofisa Elimu ya watu wazima Msingi na nje ya mfumo rasmi, amesema chimbuko la maadhimisho hayo yalianza mwaka 1975, ambapo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliona ni vyema watu wake wapate elimu kwani idadi kubwa kwa wakati huo walikuwa hawajui kusoma wala kuandika.
Mhagama amesema Tanzania kama ilivyo nchi nyingine duniani, imekuwa ikiadhimisha juma la elimu ya watu wazima kila mwaka huku shabaha yake kuu ni kuhamasisha jamii nzima kutambua nafasi ya elimu kwa kila mtu bila kujali umri, jinsia na hali ya maisha.
“Hii inajidhihirisha kuwa elimu ni endelevu na haina kikomo,ni urithi wakudumu kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla,”amesema Mhagama.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,Afraha Hassani amesema dhana ya kukuza kisomo katika dhama za kidigitali imekuja kwa sababu katika maisha ya jamii , mazingira yamebadilika, hali ya hewa imebadilika, mifumo ya kiuchumi imebadilika huku milipuko ya magonjwa inaongezeka.
“Vyote hivi vinaitaka jamii iendelee kusoma ili kupata elimu ya kukabiliana navyo,bila kujali utoto hadi utu uzima.Hivyo jamii ibadilike iendane na sayansi na teknolojia,”amesema Hassani.

Hassani ameagiza kila kijiji na kitongoji ambacho kina watu wazima wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu, kuhakikisha madarasa yao yanafunguliwa huku kwa wanafunzi waliocha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito warudi shule kuendelea na masomo ili watimize ndoto zao.
Maadhimisho hayo ya kilele cha wiki ya elimu ya watu wazima yalipambwa na maonesho ya fani mbalimbali kutoka katika vyuo na taasisi za serikali na zisizo za serikali huku yakisindikizwa na kauli mbiu isemayo “kukuza kisomo katika zama za kidigitali kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu”.

More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro