November 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wagonjwa waeleza kilio chao kwa RC juu ya kufanyishwa usafi

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Sumbawanga

MKUU wa mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amewaonya baadhi ya watumishi wa Idara ya afya Mkoani humo kuacha tabia ya kuwapa kazi za usafi wagonjwa wanao kwenda kupata matibabu wakimaliza ndipo wanawapa huduma wanazo hitaji. 

Onyo alilitoa Jana alipokuwa katika zahanati ya Kijiji cha Nambogo kilichopo katika Manispaa ya Sumbawanga alipokuwa amekwenda katika ziara ya kutatua kero mbalimbali za wakazi wa Kijiji hicho.

Alipokuwa katika Kijiji hicho, mmoja wa wakazi hao, Maria Katasha alimlalamikia mkuu huyo wa mkoa kuwa katika zahanati hiyo kumekuwa na mtindo ambapo mgonjwa akifika anapewa kwanza vifaa vya kufanyia usafi na kupewa eneo asafishe kwanza akimaliza ndipo anapata matibabu. 

“mkuu wa mkoa sisi tunashangaa hapa hospitali yetu tunakuja na mgonjwa au anakuja mtu ni mgonjwa akifika anapewa jembe apalie na kufanya usafi maeneo ya hospital akimaliza ndipo anapewa sasa matibabu”

“Unakuta  sisi wengine ni wakina mama unakesha usiku kucha na mtoto analia kwakua anaumwa hulali, ukifika hapa hospital badala ya kutibiwa unapewa eneo ufanye kwanza usafi… kitendo hiki kinatuudhi sana kwakweli tunaomba uwaeleze waache tabia hiyo labda wewe watakuelewa”

Kwaupande wake mkuu wa mkoa huyo alimuuliza mganga mkuu wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Sebastian Siwale alikiri kupokea malalamiko hayo na kusema kuwa tayari amekwisha anza kuchukua hatua kwa kufanya uchunguzi.

Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa alikemea kitendo hicho na kumuagiza Afisa utumishi kuwaondoa watumishi hao katika kituo hicho na atajua yeye kwa kuwapeleka kwakua hataki katika vituo vya afya na zahanati za mkoa huo kuwa na watumishi wanaofanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu.

Alisema kuwa baadhi ya watumishi ndio wanaharibu Nia njema ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan ya kuboresha huduma katika sekta ya afya na kamwe yeye binafsi hatawavumilia watu hao katika mkoa wa Rukwa.