Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
KWA mara nyingine, Mashujaa wa Saratani nchini wamepata fursa ya kukaa pamoja, kupata uzoevu kuhusu ugonjwa huo na pia kusikiliza nasaha kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo, viongozi wa serikali.
Kama ilivyo kawaida yao, Jumapili ya kwanza ya Juni kila mwaka huadhimisha kilele cha siku yao ya kishujaa.
Kiongozi wao anaielezea hii siku kuwa ni kusheherekea kama ilivyo sherehe za kijamii mfano kuzaliwa na ndoa.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Shujaa Foundation (SCF), Gloria Kida alisema hoja hiyo inatokana na kauli mbiu ya mwaka huu: “Sheherekea maisha.”
Aliwataka wagonjwa wasaratani waachane na hisia kwamba kuugua ugonjwa hio ni tiketi ya kifo na badala yake kuamini kuwa watapona na kupata tena fursa ya kuendelea kuishi maisha ya kawaida.
Aliwasisitizia kuitumia siku hiyo ya mashujaa kusheherekea na kubadilishana uzoefu wa kukabili changamoto zote zinazowakabili.
Katika maadhimisho ya kilele cha siku hiyo, mashujaa wa saratani pamoja na wakazi wengine wa Dar es Salaam, wakiwamo pia viongozi wa taasisi na serikali walikutana katika viwanja vya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) saa 12, asubuhi.
Tukio hilo linaanza kwa matembezi mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kurejea viwanja vya ORCI ambako walisikiliza hotuba mbalimbali za viongozi wa asasi za kiraia pamoja na serikali.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo ambayo aliwakilishwa na Kamimu Mkurugenzi wa ORCI, Dkt Mark Mseti.

Akisoma hotuba ya Mhagama, Dkt Mseti alisema serikali inaahidi kuendelea kushirikiana na mashujaa hao na kuhakikisha huduma za uchunguzi na tiba zinaendelea kuboreshwa nchi nzima.
Pia akaahidi kushirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kujenga hosteli itakayosaidia wagonjwa wanaolazimika kwenda kupatiwa huduma ORCI.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Kida kuitaka serikali kuangalia uwezekano wa kujenga hosteli maalumu kwa wagonjwa na ndugu wa familia za wagonjwa mabao wanasafri hadi Dar es salaam kwa matibabu.
Alitoa mfano wa wawagonjwa wanaosafiri tka mikoani ili kutibiwa ORCI hujikuta wanapata shida ya eneo la kulala kutokana na kushindwa kumudu gharama za nyumba za kulalala wageni.
Mbali na hilo, alisema ugonjwa wa saratani huambatana na changamoto kubwa kwenye familia ikiwa ni pamoja na kusemwa vibaya na kutengwa.
“Wapo wanaotakiwa kupata matibabu kwa muda mrefu, hii hali inakuja na changamoto kwa wagonjwa, wapo wanaofikia kwa ndugu, muda mwingine ndugu wanachoka na kuanza kuwatenga wagonjwa.
“Kuondokana na changamoto hii, serikali ijenge hosteli kwa ajili ya wagonjwa wanaotoka mbali kuja kupata matibabu Ocean Road, iwe ya bure au hata kwa kuchangia kidogo,” alisema Gloria na kuongeza.
“Wengi wanafahamu wakipata saratani wamepata kibali cha kifo, imani ambayo si sahihi. Elimu haijawafikia watu, wengi hasa vijijini. Kuugua saratani si kifo. Wengi wanatibiwa na kupona.”
***Mashujaa wakutana Besta

Shamrashamra za mashujaa hao zilianzia wiki ya mwisho ya Mei kwa ratiba mbalimbali. Mei 28, walikuwa kwenye hospitali ya Besta, iliyopo Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.
Hapa walikutana na waandishi wa habari na kuwaelezea juu ya huduma wanazozipata hospitali mbalimbali nchini, hususani hospitalini hapo.
Shujaa wa Saratani, Napendaeli Muro anaelezea kuwa mara baada ya kubainika kuwa ana saratani, aligubikwa na msongo mkubwa wa mawazo.
Miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakimsumbua kichwani ni kuamini kuwa sasa nakufa, ataugua na kuteseka kwa muda mrefu, kutojua hatma ya familia yake, hofu ya kupoteza kazi na ndoto za maisha yake kuzimika.
Lakini alipofika katika hospitali ya besta, hali hiyo ya msongo ilikwisha na kuanza kupata matumaini ya kupona na kuishi tena maisha ya furaha baada ya matibabu.
“Yaani kwa namna walivyonipokea na kunipa matumaini ama kweli nilijisikia vizuri sana,” alisema Muro.
Alielezea kuwa ndugu na hata marafiki zake walielimishwa pia jambo ambalo liliwafanya waongeze upendo na furaha juu yake.
Msimamizi wa Huduma zaTiba Hospitali ya Besta, iliyopo Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Dkt. Reuben Mringo amesema kuwa juhudi za kutibu wagonjwa wa saratani hazitumii tiba ya dawa peke yake bali ni pamoja na huduma za ushauri wa kisaikolojia kutoka kwa madaktari, wahudumu wa afya, familia na marafiki.
Dkt. Mringo alisema hospitali ya Besta imekuwa ikitumia mtindo huo na umesaidia wagonjwa wengi wa saratani kupona mapema.

“Unajua wagonjwa wengi wa saratani hupata msongo wa maisha kwamba kuugua saratani ni kufa. Tena wengi wakiandikiwa tiba ya mionzi, huamini kuwa anayepatiwatiba hiyo hufa,” alisema Dkt. Mringo akifafanua:
“Nawahakikishia tiba ya mionzi ni salama na husaidia wagonjwa wengi ila kinachochochea wagonjwa wengi wa saratani kuzidiwa na hata kufa ni msongo wa mawazo na hata kukimbia tiba sahihi hospitalini.”
Alisema hospitali ya Besta ina mfumo maalumu wa kuwatibu wagonjwa kisaikolojia kwa kuwaelimisha juu ya ugonjwa walio nao, umuhimu wa tiba wanazozitoa, jinsi ya kuishi kwa amani na matumaini ya maisha baada ya tiba.
Daktari Bingwa wa Saratani Hospitali ya Besta, Dkt. Mpibalema Yemela alisema kuwa tiba za saratani mara nyingi huwa ni za muda mrefu, hadi miaka mitano, inabidi kuwapatia elimu ya saikolojia pamoja na familia na hata marafiki.
Mratibu wa Huduma za saratani Hospitali ya Besta, Dkt. Ismail Dauda, alisema hospiutali hiyo ina vifaa vya kisasa vya uchunguzi pamoja na tiba hivyo kwa sasa hakuna haja ya mgonjwa kupelekwa nje ya nchi kwa hofu ya kutopata uchunguzi na tiba bora.
“Kitengo cha tiba ya saratani kimejitosheleza kwa huduma zote na tuna mpangilio mzuri wa kuhakikisha hakuna mgonjwa anakaa kwenye foleni muda mrefu kusubiri huduma.
“Katika maadhimisho ya mwaka huu, kama ilivyokuwa mwaka jana, tunaendelea kuhamasisha washeherekee maisha, wafurahi na wajiamini kuwa ni washindi.
“Waamini kuugua saratani siyo mwisho wa maisha na wapo wengi ambao wamepona na wameishi zaidi ya miaka 25,” alisema Kida.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu anasema ni “Sheherekea maisha” ikiwa na maana
Shujaa wa saratani ni nani?
“Katika siku hii tunamtambua Shujaa ni yule anayeishi na historia ya saratani kutoka alipogundulika mpaka baada ya matibabu. Katika siku hii tunakusanyika wote kwa pamoja kama alama ya kuonyesha jamii na dunia kuwa kuna maisha baada ya kugundulika na saratani na inawezekana,” alisema Kida akisisitiza:

“Kupitia siku hii mashujaa wa saratani duniani, alisema, wanapata nafasi ya kueleza changamoto wanazipita kuanzia wanapogundulika na saratani, wakati wa tiba na hata baada ya kupona.
“Taarifa za kitafiti zinaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la visa vipya vya saratani duniani na hata idadi ya vifo imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
“Athari kubwaya za ugonjwa ni kupunguza kwa kiasi kikubwa nguvu kazi.”
Anasema hapa nchini kumekuwa na ongezeko kubwa la visa vipya na vifo visababishwavyo na ugonjwa huu wa saratani hasa kutokana na kuchelewa kupata tiba katika hatua za awali.
MWISHO
More Stories
Hospitali ya Amana,kinara utoaji huduma za matibabu
Utafiti na Teknolojia matibabu ya magonjwa adimu wasisitizwa
Huduma ya kusafisha figo yasogezwa Manyara