Na Penina Malundo
WAZIRI wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema kati ya sampuli zilizopimwa katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii juzi (Aprili 16, 2020) na jana zinaonesha kuwepo kwa wagonjwa wapya 53 wenye maambukizi ya virusi vya Corona COVID-19 nchini, hivyo kufanya jumla ya wagonjwa hao kufikia 147.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Ummy iliyotolewa Dar es Salaam jana wagonjwa hao wote ni Watanzania.
Alisema wagonjwa ambao wameripotiwa katika Mkoa ya Dar es Salaam ni 38, Kilimanjaro mmoja, Mwanza mmoja, Pwani mmoja, Lindi mmoja, na Kagera mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo wagonjwa 10 wameripotiwa kuwepo Zanzibar. Aidha, alisema kumetokea kifo cha mtu mmoja kilichotokana na ugonjwa wa Corona nchini.
Alisema hadi sasa kuna jumla ya watu 147 waliopata maambukizi ya virusi vya Corona (COVID — 19) nchini, kati yao waliopona ni 11 na vifo 5 vimethibitishwa tangu kuanza kuripotiwa kwa ugonjwa huu nchini Machi 16, 2020.
“Wagonjwa wote waliobaki (131) hall zao ni nzuri isipokuwa wanne (4) ambao wanapatiwa matibabu ya wagonjwa mahututi kutokana na kuwa wana wanasumbuliwa na matatizo mengine ya kiafya,”alisema.
Aidha, alisema wamebaini kuwa wapo watu wenye dalili za ugonjwa wa Corona wanaokwenda kupata huduma za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Alisema hospitali hiyo ndiyo hospitali kuu ya rufaa ya kitaifa kwa wagonjwa wa magonjwa mengine nchini ambayo pia inatoa matibabu ya kibingwa na matibabu bobezi ikiwemo upasuaji mkubwa.
Magonjwa hayo ni pamoja na upandikizaji wa figo na vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto, upasuaji wa mifupa na mishipa ya fahamu na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Hivyo, alisema Serikali imeelekeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kuacha kupokea wagonjwa wenye dalili za virusi vya Corona (CODIV-19).
“Wananchi wenye dalili za ugonjwa huu wanatakiwa kuacha kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya huduma za matibabu ya corona na badala yake Serikali imeamua kutumia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Amana (Dar es Salaam) kama kituo maalum cha matibabu ya ugonjwa wa CODIV-19.
Wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wanaohitaji kupata huduma za matibabu ya magonjwa mengine katika Hospitali ya Amana wanatakiwa kutumia hospitali nyingine zilizopo mkoani hapa,” alisema.
Alitoa shukrani za dhati kwa watumishi wa afya hasa walio mstari wa mbele katika kutoa huduma katika kipindi hiki cha mlipuko wa COVID-19 nchini.
Aidha, alitoa shukrani za dhati kwa makampuni binafsi na wadau wa maendeleo kwa michango mbali mbali wanayoitoa kwa Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa huu.
“Napenda kuwakumbusha wananchi kuendelea kuzingatia na kufuatilia maelekezo ya wataalam wa afya katika kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, kuepuka misongamano na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja baina ya mtu na mtu.
Wananchi wenye dalili za ugonjwa wa Corona (COVID-19) wanashauriwa kuwahi hospitali kupata ushauri na huduma ya afya na kujitenga ili kuepuka kusambaza maambukizi kwa wengine,”alisema Waziri Ummy.
Wakati huo huo, Wizara ya Af, Zanzibar imetoa taarifa ya ongezeko la wagonjwa wapyamoja (11) wa Corona (COVID- 19) nchini na kufanya idadi ya wagonjwa hao visiwani humo kuwa 35 kutoka 24 waliotolewa taarifa Aprili 16, mwaka huu.
Taarifa ya Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed, iliyotolewa jana ilieleza kuwa wagonjwa wote hao ni Raia wa Tanzania wana historia ya kusafiri nje nchi kwa siku za hivi karibuni.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya, inaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu zinazotolewa mara kwa mara ikiwemo kuosha mikono kwa maji tiririka na sababu,” ilieleza taarifa hiyo.
Imewataka wananchi kuepuka misongamano na kuahirisha safari za nje na ndani ya nchi zisizo lazima.
Aidha Wizara imewaomba wananchi ambao wana dadili homa kali, kukohowa na kupiga chafya kujitokeza katika vituo vya Afya au kupiga simu namba 190.
“Ni vyema mgonjwa mwenye maradhi haya asijichanganye na wagonjwa au watu wengine na tuache tabia ya kujitibu wenyewe, kwani kwa kunya hivyo tutaendelea kueneza maambukizi na vifo vinavyo husiana na ugonjwa huo,”alisema.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo