Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Afya nchini imetoa taarifa ya uwepo wa wagonjwa wapya 29 waliothibitika kuwa na Virusi vya Corona (COVID-19) hivyo kufanya idadi ya wagonjwa wote nchini kufikia 88.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa wagonjwa hao ni kwa mujibu wa sampuli zilizopimwa katika Maabara ya Taifa juzi na jana.
“Wagonjwa hawa wote ni Watanzania, kati yao 26 wapo Dar es Salaam, wawili Mwanza na mmoja Kilimanjaro na wote wanaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa wataalam wa afya,” ilieleza taarifa hiyo na kuongeza;
“Ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu na wagonjwa hawa (Contact Tracing) unaendelea.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo hadi kufikia jana jumla ya watu 88 wamepata maambukizi ya COVID-19 nchini kutoka 53 waliotolewa taarifa awali.
“Ongezeko hili la wagonjwa linajumuisha wagonjwa wapya sita waliotolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar mapema leo.
Aidha wagonjwa waliopona hadi jana ni 11 na vifo vitokanavyo na COVID-19 nchini ni vinne.
Serikali inaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kama wanavyowapatiwa taarifa na elimu mara kwa mara kupitia njia mbali mbali.
Taarifa hiyo imewataka watu katika kipindi hiki kuepuka misongamano na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.
More Stories
Jay-Z aunganishwa na P Diddy kwa kumdhalilisha binti wa miaka 13
Rais Samia afanya uteuzi
Waliombaka, kulawiti binti wa Yombo, Dar jela maisha