Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
ZAIDI ya wagonjwa 500 wanatarajiwa,kupata matibabu ya kibingwa ya mtoto wa jicho, kwa siku saba katika hospitali ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya,huku lengo ni kupunguza tatizo la upofu nchini hapa.
Kambi hiyo ya matibabu ya macho inaratibiwa na Shirika la Helen Keller International (HKI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.
Akizungumza na washiriki wa kambi hiyo,Daktari Bingwa wa macho na Kiongozi wa timu ya wataalamu hao,Dkt. Barnabas Mshangila,amesema kuwa kambi hiyo inatoa fursa kwa wagonjwa wengi ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya mtoto wa jicho,ambapo watawafanyia upasuaji.
“Tumejipanga kwa kila hali,tunatarajia kutoa huduma bora kwa wagonjwa wetu. Ni muhimu kuhakikisha kwamba kila mtu anayehitaji huduma za macho anapata matibabu stahiki,”Dkt. Mshangila
Mratibu wa huduma za macho Mkoa wa Mbeya Dkt. Fariji Kilewa, amesisitiza kuwa huduma kama hizo ni muhimu kwa jamii,hivyo amewashukuru wadau wote wanaohusika katika kutekeleza mradi huu.
” Ushirikiano wa pamoja unasaidia kufanikisha malengo yetu ya kutoa matibabu bora kwa wagonjwa wa mtoto wa jicho,”amesema.
Kwa upande wake,Ofisa Mradi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Helen Keller,Allen Lemilia,amesema shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,katika kuboresha huduma za matibabu ya macho kwa wananchi walio maeneo ya mbali.
Pia maeneo ya kutolea huduma za afya kwa kufanya huduma mkoba,kwa kupeleka wataalamu pamoja na vifaa tiba vya kutolea huduma,ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kupunguza gharama kwa jamii na kupunguza tatizo la upofu mkoani Mbeya.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais