January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wagonjwa 200 wa ngiri maji,ngiri kokoto kufanyiwa upasuaji

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

Wagonjwa 200 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na Mtama wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa ugonjwa wa ngiri maji na ngiri kokoto kupitia kambi ya upasuaji ilioanza Oktoba 2 hadi Oktoba 13 mwaka huu.

Kambi hiyo ambayo inawezeshwa na kampuni ya Nishati ya Kimataifa ya Equinor Tanzania (AS) kupitia Programu ya Taifa ya Magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTD) ambayo ni maalumu kwa ajili upasuaji kwa wagonjwa wa ngiri maji na ngiri kokoto.

Ofisa kutoka Kampuni ya Equinor Tanzania Dkt. Naomi Makota, akitoa ufafanuzi kwa Maofisa wa PURA, waliofika katika kambi hiyo, amesema kuwa upasuaji umeanza rasmi Oktoba 2, mwaka huu na kutarajiwa kuhitimishwa Oktoba 13 ambapo wanaatarajia kufikia idadi hiyo ya wagonjwa.

Dkt. Naomi ameeleza kuwa huu ni mwaka wa 9,tangu kampuni hiyo ianze kufadhili Programu ya NTD na kufanikisha upasuaji wa wagonjwa hao.

Pia ameeleza kuwa, tangu kuanza kwa utekelezaji wa programu hiyo zaidi ya wagonjwa 1,600, wa ngiri maji na ngiri kokoto wamefanyiwa upasuaji ambapo hadi sasa mradi huo umegharimu takribani Dola za Marekani 424,400.

Kwa upande wake Ofisa kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Ebeneza Mollel, amesema kuwa kampuni hiyo imerudisha tabasamu kwa wagonjwa wa ngiri maji na ngiri kokoto, wanaopata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi-Sokoine.

“Kwa ufadhili huu wa upasuaji huu hakika mradi huu unabadilisha maisha ya wagonjwa na tumeguswa sana na mchango wa Equinor katika eneo hili”,amesema Mollel.