December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya madaktari wa hospital ya Rufaa ya Kanda wakizungumza na waandishi wa habari leo mkoani mbeya.

Wagonjwa 19 wafanyiwa upasuaji wa midomo wazi,uvimbe wa taya

Na Esther Macha,TimesMajira,Online, Mbeya.

WAGONJWA 19 wamefanyiwa upasuaji wa midomo wazi, uvimbe wa taya na kuvunjika kwa taya huku  kati yao watoto wakiwa  sita na mmoja akiwa amezidi miaka 60.

Wagonjwa hao wamepata huduma hiyo katika maadhimisho ya miaka 40 ya Chama cha Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno nchini (TDA) yanayoadhimishwa mkoani Mbeya yaliyoanza  Novemba 16 hadi 27 mwaka huu.

Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari mkoani Mbeya katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Katibu wa Chama hicho, Dkt. Gemma Berege amesema wagonjwa hao walifanyiwa upasuaji kati ya novemba 16 hadi 20 mwaka huu walipofika katika maadhimisho hayo.

Amesema maadhimisho hayo ni  ya miaka 40 ambapo yanafanyika kwa  mara ya kwanza mkoani humo huku kukiwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wanaoshiriki.

Aidha amesema wanategemea kupata wagonjwa wengi  kutokana na mwitikio huo kuwa  mkubwa ambapo Novemba 23,mwaka huu wataalamu hao wanatarajia kutembelea baadhi ya Shule jijini Mbeya na kupima afya ya kinywa kisha kuwafanyia matibabu ambapo matibabu hayo yatakayofanyika Novemba 24,2020 katika uwanja wa Chuo cha Uhasibu (TIA).

Kwa upande wake Dkt. Njama Shekallaghe ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo amesema Wataalamu hao pia watatoa elimu kisha watafanya kongamano la miaka 40 na kumalizia kwa mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, Dkt. Lazaro Mboma amesema maadhimisho hayo yamekuja katika muda muafaka ambapo wagonjwa wengi wananufaika na huduma za bure kutoka kwa wataalamu hao.

Baadhi ya wanufaika wa matibabu hayo wamesema maadhimisho hayo kufanyika mkoani humo  wamepata manufaa makubwa bila gharama yoyote.