Na Allan Kitwe,Timesmajiraonline,Tabora
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijiandaa kuanza vikao vya ndani vya mchujo wa majina ya wagombea walioomba nafasi ya udiwani na ubunge, watia nia wote wametakiwa kutochafuana kwa kuwa wote wana nafasi sawa ya uteuzi.
Onyo hilo limetolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Komredi Wilson Nkambaku alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili Ofisini kwake.
Amewapongeza wanaCCM wote waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama kuwania nafasi za udiwani wa kata na ubunge wa majimbo ikiwemo nafasi za viti maaalumu kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Nkambaku amesisitiza kuwa watia nia wote wana haki sawa za kuteuliwa na chama katika nafasi hizo, hivyo akawataka kuwa watulivu katika hatua hii ambapo vikao vya chama vinaanza mchujo wa awali kupitia majina ya wagombea wote.
“Naomba watia wote mheshimiane, msichafuana kwa maneno yasiyofaa, kwa kuwa hakuna ajuaye kama jina lake litarudi au halitarudi, vikao vya chama vitaamua kwa haki, mwenye sifa na vigezo vinavyotakiwa atateuliwa,”amesema.
Ameeleza kuwa chama kinawathamini sana wanachama wake waliotia nia, hivyo akawataka kuwa watulivu na kuviachia vikao vya uteuzi kufanya kazi yao, majina matatu yatakayopitishwa yataletwa ili kupigiwa kura na wanachama.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Daniel Mhina amesema kuwa watia wote ndani ya Chama Cha Mapinduzi wana haki sawa ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama na hata kama hutateuliwa bado chama kinawathamini sana.
Amesisitiza kuwa vikao vya uteuzi vitazingatia zaidi sifa na vigezo visivyotia shaka kwa watia wote na hata ikibainika kuwa wote wana sifa sawa, vikao vitaangalia sifa za ziada ili kupata majina matatu yatakayoletwa kwa wanachama.
Mhina amedokeza kuwa chama kiko makini na wajumbe wa vikao wana uwezo mkubwa wa kuona ni nani anayefaa kuteuliwa ili kukiwakilisha kwa wananchi katika uchaguzi unaoshirikisha vyama vingine vya siasa.



More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi