January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waganga wakuu wa wilaya waonywa

Na Mathew Kwembe, Morogoro

SERIKALI imewataka waganga wakuu wa wilaya nchini kuhakikisha kuwa wanawasimamia watendaji wa vituo vya kutolea huduma za afya kuweka kumbukumbu za dawa, vifaa tiba, vitendanishi vinavyonunuliwa pamoja na mapato yatokanayo na huduma hizo.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt.Festo Dugange wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Mvomero.

Amesema, kuanzia sasa hatarajii kuona kituo cha kutolea huduma ya afya hakina kumbukumbu ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba pamoja na taarifa za mapato ya kituo husika cha kutolea huduma za afya.

Agizo la Naibu Waziri linafuatia ziara yake katika Hospitali ya Wilaya ya Mvomero na kukuta Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo kushindwa kueleza kumbukumbu za dawa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na mapato ya hospitali hiyo licha ya hospitali hiyo kuwa na dawa zote muhimu zinazohitajika.

Amesema, Serikali haipo tayari kuona mali inazonunua zinapokelewa na zinatumika bila kuwa na kumbukumbu zinazotakiwa.

“Tukifika katika kituo tukute mtiririko wote wa kumbukumbu zote umeainishwa, wahusika wamesaini, na hizo dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinaonekana na kama vimetumika tunajua nani ametumia,”amesema.

Alisema, Serikali inapotaka kununua dawa asihusike mtu mmoja peke yake maamuzi ya dawa zipi zinunuliwe, za shilingi ngapi, zinanunuliwa wapi, maamuzi yafanywe na kamati ya matibabu ya kituo ambayo ina wajumbe kadhaa, ambao watasaini na kukubaliana kuwa inakwenda kununua dawa hizi.

“Dawa zikishanunuliwa ni lazima zipokelewe na wajumbe wale, wazihesabu, wajiridhishe, waweke na saini zao kwamba tumepokea dawa hizi,”amesema.

Dawa hizi ziingizwe kwenye leja na zinapotoka bohari kuu ziende kwenye bohari ndogo na kwenda kwa mgonjwa ili kila sehemu nani alizitoa hapa na kuzipeleka dispensing, akapeleka kwa wagonjwa nani ni mgonjwa gani alipata zile dawa.

“Bado sijaridhishwa na ufanisi wa makusanyo ya huduma za uchangiaji. Mganga mfawidhi hujui kwa siku anakusanya shilingi ngapi, katika seksheni ipi tunachotaka kila sehemu ijipime, maabara ijipime wao wanachangia kiasi gani kwa siku, kwa mwezi na kwa mwaka, dawa wajipime, wodi ya watoto wajipime, kwa sababu hivyo vyote ndiyo vyanzo vya huduma, lakini pia ndiyo vyanzo vya mapato.

“Ni lazima tuondoke kwenye mentality ya utegemezi sana. tumekwishakubaliana katika mamlaka za serikali za mitaa sekta ya afya iwe na uwezo wa kusimama kwa miguu yake ikisaidiwa na fedha kutoka serikali kuu,” amesema na kuongeza.

“Tusiwe wategemezi asilimia 99 ya fedha ya serikali kuu, ya MSD haiwezekani, kwasababu sisi tunazalisha, tunatoa huduma, tunachangiwa huduma ya fedha lazima fedha zile zionekane ni kiasi gani kwa siku, zimekwenda wapi, zinatumika wapi. Hili nimewapa siku 21, nataka nije nione taarifa kabisa ambayo inaeleza kila seksheni inachangia kiasi gani.

Lakini pia nimeona hamuingizi fedha benki kwa wakati na ninyi benki ipo hapa ndani ya mita kadhaa, lakini ninyi kwa mwezi kwa mfano mei mmeingiza mara 6 tu katika siku 31, siku 25 fedha zilizokusanywa zinakwenda wapi.

“Namuagiza mganga mkuu wa wilaya ya mvomero, mganga mfawidhi, nataka nipate taarifa ya mapato ya mwezi wa tano wote yaliyokusanywa hapa ambayo yatakuwa na ushahidi kwenye mfumo na nikiwa na mashaka nitarudi, na nikiona mmetoa taarifa isiyo sahihi hali yenu haitakuwa nzuri.

Pia apate taarifa ya mapato ya hospitali kwa mwaka mzima mnapata shilingi ngapi kwa wastani, Januari hadi mwezi wa sita mnapata shilingi ngapi kila mwezi na hili nataka liwe endelevu. Hakuna jambo tunahitaji kusisitiza kama kuhakikisha tunaziba mianya ya upotevu wa fedha za serikali.

Aidha amesema Kuna baadhi ya watumishi wa serikali wasio waaminifu wanatumia vibaya fedha zetu za makusanyo katika vituo vyetu vya kutolea huduma na wanapelekea vituo hivyo kuwa na fedha kidogo , hawawezi kujiendesha kwasababu tu ya kutokuwa waaminifu.

“Misamaha inasingiziwa sana pamoja tunajua tuna mzigo wa msamaha lakini kuna feki exemption nyingi.

Hakuna mifumo mizuri ya kuratibu nani anastahili kusamehewa na kweli amesamehewa, wapo baadhi ya watumishi wachache ambao wanatumia fursa ya misamaha kudanganya, kujipatia mapato ya udanganyifu na wanaandika kwamba hii ni misamaha.

Nielekeze na nitalifuatilia kwa karibu sana nataka tukiambiwa hii ni misamaha tuone ipo wazi kwamba ni misamaha na ni nani tukitaka kumtrace mnufaika wa msamaha tumpate,”amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Albinus Mgonya alimuhaidi Naibu Waziri kuwa maagizo yote aliyoyatoa yatatekelezwa na taarifa atazipata ndani ya siku 14 badala ya 21 kama alivyoagiza Naibu Waziri.