Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
MAAMUZI ya Serikali kuanzisha mradi wa upelekaji umeme vijijini maarufu kwa jina la “Umeme wa REA” yametajwa kuwa na mafanikio makubwa kutokana na nishati hiyo kutoa fursa nyingi za ajira vijijini.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kuipongeza Serikali huku wakiomba kuongezwa kwa kasi zaidi ya upelekaji umeme kwenye maeneo yote ambayo hayapata huduma ya umeme.
Baadhi ya vijana wamesema kupatikana kwa umeme katika maeneo yao wameweza kunufaika kwa kujiajiri wenyewe katika fani za ufundi wa uchomeleaji wa vyuma na wengine kuanzisha miradi ya mashine za usagaji nafaka.
Kwa upande wao Faida Meshack, Godfrey Alex wakazi wa kijiji cha Solwa Shinyanga na Charles Yatabu na Paulo Ngudungi wakazi wa kata ya Iboja, Ushetu Kahama wameishukuru Serikali kwa kuanzisha mradi huo wa REA ambao umewakomboa vijana wengi waliokuwa na changamoto ya kupata ajira.
Nao baadhi ya maofisa watendaji wa kata na wale wa Vijiji (VEO) Mihambo Kizito kata ya Jana, Kahama, Satto Mayungu kata ya Solwa na Jesse Malima ambaye ni Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Solwa na mwenyekiti wake wa kijiji, Masindi Lusoloja wameishukuru Serikali kwa mradi huo wa REA.
Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo mbali ya kuishukuru Serikali kwa kuwapatia zabuni ya utekelezaji wa mradi huo lakini pia wameahidi kufanya kazi zao kwa kuzingatia mikataba waliyopewa ili wakamilishe kazi kwa wakati ambao umepangwa.
Mhandisi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini TANESCO Mkoani Shinyanga, Anthony Tarimo amesema mkoa wa Shinyanga una vijiji 509 katika halmashauri zake sita ambapo awamu ya kwanza ya usambazaji umeme wa REA ilianza mnamo mwaka 2013 kwa awamu tofauti tofauti.
Mhandisi Tarimo amesema katika awamu hiyo ya kwanza jumla ya vijiji 15 vilinufaika na mradi huo katika wilaya za Kahama na Shinyanga ambapo awamu ya pili vijiji 49 vilifikiwa na huduma hiyo kwa wilaya zote za mkoa wa Shinyanga na hivi sasa awamu ya tatu jumla ya vijiji 136 vimenufaika na mradi huo.
“Mpaka hivi sasa baada ya kukamilika kwa mradi wa awamu ya tatu mzunguko wa kwanza vijiji 262 vimenufaika na umeme huo na vijiji 247 vilivyobaki vipo kwenye mchakato na vingine vinaendelea kupatiwa umeme kwenye mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili,” anaeleza Mhandisi Tarimo.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime