March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafugaji watakiwa kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la chanjo

Na Esther Macha,Timesmajira Online,Mbeya

KATIKA kuhakikisha mifugo inachanjwa wafugaji wametakiwa kutoa ushirikiano  wa karibu  kwa maafisa mifugo wa kata ili kuweza kufanikisha zoezi hilo pasipo vikwazo.

Hayo yamesemwa Agosti,18,2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Dinday Njile aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo  wakati wa uzinduzi wa kampeni ya  utoaji chanjo kwa mifugo.

Amesema katika kufanikisha zoezi hilo wafugaji wote wanapaswa kuchanja mifugo yao na kutoa ushirikiano pindi maafisa mifugo wa kata wanapofika katika maeneo yao ili kurahisisha kampeni ya  kuchanja mifugo iweze kufanikiwa pasipo changamoto yeyote.

“Kampeni hii ya utoaji chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, imeanza Leo katika Kata ya Mjele kijiji cha Chang’lombe Wilaya ya Mbeya imani yetu wafugaji wote mtazingatia zoezi hili muhimu “amesema .

Pia Njile amewatoa hofu wafugaji kuwa zoezi hilo ni endelevu na litaendelea kwa kipindi cha miaka mitano, hivyo hawapaswi kuwa na wasiwasi.

Hata hivyo amesema Serikali imesikiliza changamoto zinazowakabili wafugaji na tayari imeanza kuzifanyia kazi kwa maslahi ya sekta hiyo muhimu ya mifugo.