January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyakazi wanawake watoa msaada kwa watoto

Na Penina Malundo,timesmajira,online


Wafanyakazi wanawake kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) kwa kushirikiana na Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) pamoja na Kampuni ya Uzalishaji wa Nguzo za Zege (TCPM) ambazo zote ziko chini ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),wametembelea hostel ya watoto wanaougua ugonjwa wa saratani jijini Dar es Salaam na kukabidhi msaada wa mahitaji muhimu.
Msaada huo wa mahitaji muhimu uliokabidhiwa kwa watoto hao, ni pamoja na dawa, vifaa tiba, vyakula, vifaa vya kufanyia usafi ambavyo kwa pamoja vimegharimu kiasi cha shilingi milioni tatu (3,000,000).
Akiongea baada ya kukabidhi msaada huo, Afisa Rasilimali watumishi wa TANESCO, Judith Gowele amesema, katika kusherehekea siku ya wanawake, wao kama wafanyakazi wanawake hujumuika pamoja na watu wenye uhitaji na kwa mwaka huu wameona wajumuike na watoto wanaougua saratani na kuwapa mahitaji muhimu. 
Amesema  kuwa, kwa kufanya hivyo, ni kuonesha ishara ya upendo, kujali na uthamini si kwa watoto tu, hata kwa wazazi, walezi na wahudumu wa afya wanaowahudumia watoto hao. 
“Katika kusherehekea siku ya wanawake tumeona ni fahari kwetu kujumuika na watoto wanaougua saratani, kuendelea kuwaonesha upendo, kuwathamini na kuwajali ili waendelee kujiona ni sehemu ya jamii sawa na wengine” amesema  Gowele 
Gowele ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi wa watoto hao kutokata tamaa, kuwa na imani na kuendelea kumuomba Mungu kwani changamoto hiyo inaweza kumkuta mtoto yeyote na mzazi yeyote. 
Kwa upande wake, Mtaalam wa Mfumo wa Taarifa za Kijiografia (GIS) kutoka TGDC, Anastacia Ndmbo, amesema kuwa, kitendo cha kukaa hospitali wiki, mwezi au mwaka ni gharama kubwa sana kwani Kuna utaratibu mwingine wa maisha unasimama, na hivyo ametoa rai kwa makundi mengine kujitokeza kusaidia wenye uhitaji hospitalini ikiwemo watoto hao. 
“Kukaa hospitali wiki, mwezi au mwaka ni gharama sana na inaumiza, mbali na kukabidhi misaada yetu, nitoe rai kwa mtu mmoja mmoja na makundi ya kijamii pamoja na taasisi kujitokeza kusaidia watu wenye uhitaji na huo ni moyo wa upendo sawa na maandiko katika vitabu vya dini” amesema Ndimbo

Maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani yalianzishwa mwaka 1908 na kwa sasa yanaadhimishwa kwa mwaka wa 101, ambapo kitaifa siku ya Wanawake Duniani itaadhimishwa Machi 08, katika ukumbi wa mikutano Mlimani City jijini Dar es Salaam huku kauli mbiu yake ikiwa ni ‘Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu’