Na Reuben Kagaruki,TimesMajira,Online,Dar
WASICHANA wanaofanyakazi za ndani jijini Dar es Salaam wametaja sababu zinazochangia vitendo vya ukatili wa kingono baina yao na waajiri wa kiume na sababu za vitendo hivyo kuanikwa waziwazi.
Wafanyakazi hao wa ndani waliweka wazi sababu hizo wakati wakizungumza kwenye semina ya kuwajengea uwezo iliyoandaliwa na Taasisi ya Sauti ya Jamii Kipunguni kupitia ufadhili wa Tanzania Women Trust Fund ya jijini Dar es Salaam jana.
Wametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa mikataba ya kazi na elimu ya kujitambua imekuwa moja ya wao kujiingiza kwenye vitendo vya ngono na waajiri wa kiume.
Wametaja sababu nyingine kuwa ni kukosekana kwa mikataba ya ajira za kazi wanazofanya, hivyo baadhi yao hulazimika kutoa rushwa ya ngono kwa waajiri wao wa kiume ili kulinda kazi zao
Latifa Mussa mkazi wa Chanika ambaye alikuwa ni mmoja wa wasichana aliyeshiriki mafunzo hayo, amesema vitisho wanavyopewa baadhi ya wasichana na mabosi zao wa kiume vinasababisha kutoa rushwa ya ngono
“Wakati mwingine tumekuwa tukijaribu kukataa kushiriki mapenzi na mabosi zetu wa kiume, lakini wamekuwa wakitupa vitisho na kulazimika kushiriki nao bila kupenda,”amesema Mussa.
Amesema elimu ya kujitambua inahitajika kwa wasichana wa kazi ili kuwawezesha kuwa na maamuzi sahihi juu ya mustakabali wa maisha yao hususan kipindi hiki ambacho kumekuwa na magonjwa mengi ya kuambukiza
Mariam Mussa amesema mbali na vitendo hivyo kufanywa na mabosi zao wa kiume, pia waajiri wakike wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kutokuwa karibu na wasichana wao wa kazi, huku wengine wakiwa wakali sana
“Ukijaribu kutaka kumueleza bosi wako wa kike kuhusu mwenendo mbaya anaotaka kuufanya bosi wa kiume kesi yote inahamia kwako, ukiangalia una shida na kazi na hivyo kujikuta ukilazimika kutoa rushwa ya ngono ili kulinda kibarua,”amesema Mussa
Amesema ipo haja kwa wanawake kutambua mipaka ya kazi za wasichana, kwani baadhi wamekuwa wakijisahau na kumuacha msichana akifanya majukumu mazito anayopaswa kufanya mama na kumuingiza kwenye matatizo ya rushwa ya ngono
Kwa upande wake, Mratibu na Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishagazi alisema semina hiyo ni muendelezo wa kampeni ya kuzuia rushwa ya ngono kwa wasichana wa kazi za ndani ili waweze kuvunja ukimya wa masuala hayo na kuwawezesha kuripoti vitendo hivyo kwenye mamlaka husika
“Huu ni muendelezo wa kampeni za kuzuia rushwa ya ngono kwa wasichana wa kazi za ndani na wanawake, wasichana wenye ndoto za kuwa viongozi zibazofanywa na Taasisi ya Sauti ya Jamii Kipunguni,”amesema Bishagazi
Aidha, ameongeza kuwa Sauti ya Jamii Kupunguni imekuwa ikitoa elimu kwa wanawake na wasichana ili waweze kushiriki nafasi za uongozi sambamba na kudai haki
Amesema wamekuwa wakitoa elimu ya madhara ya rushwa ya ngono na umuhimu wa kuripoti vitendo hivyo kwenye mamlaka husika pamoja na kuwajibika. Hata hivyo, Bishagazi alisema miaka kadhaa sasa imepita wafadhili mbalimbali Sauti ya Jamii Kipunguni imekuwa ikiendesha semina za aina hiyo kwa wasichana wanawake na kupata matokeo mazuri ikiwepo baadhi yao kuamua kuvunja ukimya na kuripoti vitendo hivyo kwenye mamlaka husika
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu