December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Leonard Subi

Wafanyabishara waomba kupatiwa elimu ya magonjwa ya mlipuko

Na Joyce Kasiki,TimesMajira,Online

WAFANYABIASHARA wa mbogamboga na matunda katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma,wameomba mamlaka zinazohusika kuwapatia elimu juu ya kujikinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao wamesema,kutokana na biashara wanayoifanya upo umuhimu mkubwa wa kupatiwa elimu hiyo ili wajikinge wao pamoja na wateja wao.

Abdallah Juma Muuza wa Matunda amesema kuna baadhi yao wamekuwa wakifanya biashara zao bila kuzingatia usafi hali ambayo kwa kiasi kikubwa inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama vile kuhara na kipindupindu.

“Biashara ninayofanya mimi ni ya matunda ambapo tunamenya,tunayakatakata kabisa  na kuyaweka kwenye sahani,mteja akija kununua moja kwa moja anaanza kula,kwa hiyo utaona kabisa jinsi biashara hii inavyotaka usafi,lakini wengi wetu bado uelewa kuhusu masuala ya usafi ni mdogo sana.” Amesema Abdallah

Mfanyabiashara mwingine Kenned Massawe pia amesema,kuna baadhi yao hawazingatii kabisa suala la usafi hali ambayo amesema inahatarisha afya za wananchi.

“Nikiri tu kwamba tunahitaji tupatiwe Elimu,ili tufanye biashara zetu kwa usafi wa hali ya juu,” amesema Kenned

Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto  Dkt.Leonard Subi wakati akijibu maombi hayo ya wafanyabiashara, amesema katika kuhakikisha kundi la wafanyabiashara hususani wa vyakula wanakuwa salama na kuepukana na magonjwa ya mlipuko,Serikali imejipanga kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kupitia vyombo mbalimbali vya habari zikiwemo radio na televisheni ili kuhakikisha elimu inawafikia kwa ufasaha.

 Aidha amewaagiza maafisa afya nchini kote kuhakikisha wanakagua  mazingira ikiwemo ya wafanyabiashara mbalimbali,na maeneo yote ya mikusanyiko ili yawe safi kuepukana na magonjwa ya mlipuko.