Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Wafanyabiashara wa soko kuu jijini Mwanza,wamewatoa hofu wananchi wa mkoa huo juu ya kupanda kwa bei ya vyakula na bidhaa mbalimbali katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Huku wito ukitolewa kwa wafanyabiashara nchini kuacha tabia ya kutumia mwezi huo wa Ramadhani kama fursa ya kujipatia faida mara dufu kwa kuongeza bei ya bidhaa mbalimbali.
Wakizungumza na Majira sokoni hapo Februari 17,2026, baadhi ya wafanyabiashara hao wameeleza kuwa wananchi wanapaswa kutambua kuwa bei za vyakula au bidhaa hupanda kutokana na bei ambayo hulangua bidhaa hizo tofauti na dhana iliopo ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo,Khadija Abdallah,alisema,wafanyabiashara wa soko hilo hawataraji kupandisha bei katika mwezi huo wa Ramadhani.
Alisema kwa sasa dagaa kisado anauza shilingi 10,000, lakini hata kwa soko zima bei ni hiyo hiyo lakini hatarajii kusikia kuwa kuna mtu atapandisha bei ya vyakula.
“Wananchi wasiogope kuja kununua bidhaa sokoni kwetu,na wakikuta bei ipo juu mfano kwa sasa kilo ya sukari ni 2,800,wakikuta sukari inauzwa shilingi 3,000, anaweza kupiga picha na uzuri meza zina namba na kwenda kushitaki serikalini ili hatua zichukuliwe,”alisema Khadija.
Naye Amani Jonas,aliwatoa hofu wananchi juu ya kupanda kwa bei ya vyakula huku akisisitiza kuwa bei hupanda kulingana na namna mfanyabiashara anavyouziwa kwa bei ya jumla.
“Kwa sasa bidhaa zinazotumika kwa wingi kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani zipo vizuri kwani mchele kilo wa bei ya chini ni shilingi 2,500 na juu zaidi ni shilingi 3,500, maharage kilo shilingi 2,000 huku nyuma yalikuwa shilingi 2,500 hadi 3,000 na wananchi watarajie kuwa bei haitapanda na wasiwe na hofu,”alisema Jonas.
Mwenyekiti wa soko kuu jijini Mwanza,Hamadi Nchola,alisema bidhaa za vyakula kwa upande wa mchele zipo za aina tatu,ambapo kilo moja ya mchele wa kiwango cha juu(grade one) kwa sasa unauzwa kwa shilingi 3,500,wa kati sh. 3,200 na wa chini sh.2,800 kwa kilo.
“Bei ya mchele kwa sasa ipo juu kulinganisha na Januari kurudi nyuma ambapo kilo ya mchele kiwango cha juu ni shilingi 3,000, wa kati sh.2,800 na WA kiwango cha chini sh.2,000.Sababu za sasa mchele kupanda ni akiba za wakulima kupungua na siyo Kwa ajili ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani,
Pia amesema sababu ya bei ya mchele kupanda ni kutokana na hali ya joti na mvua kuwa chache hali ilisababisha wakulima kuvuna kwa uchache mpunga.
Huku kwa upande wa bidhaa nyingine bei zinaendelea kushuka ambapo maharage ambayo mara nyingi yanatumika kwa wingi kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa sasa sokoni hapo yanauzwa kilo moja kwa shilingi 1,800.Ambapo kipindi kilichopita cha Januari mwaka huu kurudi nyuma kilo ya maharage ilikuwa inauzwa shilingi 2,500.
“Bidhaa nyingine ni viazi mviringo ambavyo vinatoka sehemu mbalimbali ikiwemo Mbeya, Bukoba na nchi jirani ya Rwanda,ambapo mwanzoni mwa Januari ,2026 gunia moja lilikuwa linauzwa shilingi 110,000 lakini leo ninavyoongea gunia linauzwa shilingi 95,000,”amesema Nchola na kuongeza:
“Mara nyingi mwezi wa Ramadhani vyakula ni vingi ingawa watu wengi wanakuwa na hofu kuwa vitapanda bei.Jana tulifanya kikao na Mkuu wa Mwanza Said Mtanda,alitutaka Wenyeviti wa masoko tuwashauri wafanyabiashara wasipandishe bei katika mwezi huo kwani wateja ni wale wale wa kila siku,”.
Nchola,alisema,baada ya kikao hicho leo(jana),Katibu wa soko hilo ametoa tangazo kwa wafanyabiashara sokoni hapo kuhakikisha kwamba hawapandishi bei ya bidhaa mbalimbali ikiwemo vyakula.
“Tunatarajia bei ya vyakula kushuka pia kuwa nyingi kwani baadhi ya wafanyabiashara wa soko hili wameenda kutafuta bidhaa mbalimbali za vyakula isipo kuwa mchele kwani mwaka huu mpunga umevunwa kidogo kutokana na mvua kuchelewa kunyesha,ambapo kumesababisha wakulima kuwa wagumu kuuza bidhaa kwa wafanyabiashara,”alisema Nchola.
Hata hivyo alimuomba Mungu kwa kudra zake asaidie bidhaa ziendelee kushuka bei ikiwemo maharage yafikie kuuzwa kilo moja kwa shilingi 1,200 huku akisisitiza kuwa vyakula vinaendelea kushuka bei ikiwemo magimbi na viazi vitamu.
Aidha alisema,maharage yataendelea kushuka kwa sababu wakulima wamevuna sasa hivi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Bukoba, Kigoma, Manyara.
“Wafanyabiashara wote nchini tusipandishe bei ya vyakula hata Mwenyezi Mungu amekemea hilo,pia wazalishaji wa bidhaa za viwandani kama tambi,sukari nao wasipandishe bei kwani wateja wao ni wale wale,”.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria