November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara washauriwa kusajili biashara,kampuni

Na Queen Lema,Timesmajira Online,Arusha

Wafanyabiashara pamoja na wajasiriamali hapa nchini wameshauriwa kusajili biashara pamoja na kampuni zao ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali ambazo wakati mwingine wanazikosa kutokana na kutosajili majina ya biashara na kampuni.

Hayo yameelezwa na Ofisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili na Leseni (BRELA) Gabriel Girangai wakati akizungumza kwenye maonesho ya huduma za fedha ambayo yanaendelea jijini Arusha.

Girangai amesema kuwa mfanyabiashara anaposajili biashara inamsaidia kuweza kukutana na fursa mbalimbali ikiwemo kupata huduma sahihi na kwa wakati sahihi kutoka kwenye taasisi mbalimbali.

“Unapopata usajili unaweza hata kukopesheka kutoka katika kampuni za biashara lakini pia unawavutia wawekezaji hata kutoka nje ya nchi kuweza kufanya kazi,”amesema.

Katika hatua nyingine amesema kuwa BRELA imeweza kurahisisha zoezi zima la usajili wa biashara ambapo hufanyika kwa njia rahisi tofauti na awali.

“Kwa kujua umuhimu wa muda kwa hawa wafanyabiashara tumewarahisishia kwa kutumia mtandao wanapata kila kitu ambacho wanastaili kuwa nacho hata kama ni saa tisa usiku unapata huduma nawasihi sana wafanyabiashara kuhakikisha sasa wananufaika na huduma hizi,”.

Awali amewataka wafanyabiashara pia kuachana na tabia ya kutumia majina ya biashara ambayo siyo ya kwao na badala yake waweze kusajili wao kama wao ambapo kupitia utambuzi wa majina ya biashara na kampuni wataweza kupata fursa.