November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara wanaoumiza wakulima kwa lumbesa waonywa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dodoma

WAKALA wa Vipimo (MWA), imesema itaendelea kuwadhibiti wafanyabiashara wanaotumia lumbesa ili kuhakikisha mkulima ananufaika na kazi ya mikono yake.

WMA imeahidi kuendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza kila msimu wa mazao ili kuhakikisha mizani zinazotumika zimehakikiwa na wakulima hawaibiwi na baadhi ya wafanyabiashara.

Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka (WMA), Albogast Kajungu, katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo maarufu kama NaneNane yanayoendelea katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma.

Alisema WMA ina mchango mkubwa katika sekta ya kilimo hususani katika mazao ya kimkakati ambayo ni korosho, ufuta, kahawa, tumbaku na pamba kuhakikisha suala la vipimo lianzingatiwa na wakulima hawaibiwi.

Alisema kazi kubwa ya Wakala wa Vipimo katika sekta hiyo ndogo ya mazao ya kimkakati ni kuhakikisha mizani zinazotumika katika ununuzi wa mazao hayo zinahakikiwa ili kujiridhisha kuwa ziko sahihi.

“Lengo ni kuhakikisha kwamba mkulima anapouza mazao yake anapata thamani ya pesa sawasawa na mazao aliyouza,” alifafanua Kajungu.

Mkurugenzi alisema kazi ya kuhakiki mizani hufanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha uhakiki wa mizani kabla ya msimu wa kila zao kuanza wakati awamu ya pili inahusisha ukaguzi wa kushtukiza.

Alisema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa kushtukiza wakati wa msimu kwa kila zao ili kujiridhisha kama vipimo vilivyohakikiwa awali vinatumika kwa usahihi.

“Kwa hiyo kabla ya msimu tunapita kuhakiki mizani zote zinazotumika kununulia mazao na wakati wa msimu tunapita kujiridhisha kama zinatumika kwa usahihi,” alisema

Aidha, Kajungu alieleza kuwa, mbali na kazi ya ukaguzi, WMA hutoa elimu kwa wakulima na wananchi kwa ujumla ili wafahamu sifa za mizani ya kununulia mazao iliyohakikiwa.

Alitaja mojawapo ya sifa za mizani iliyohakikiwa kuwa ni uwepo wa stika ya WMA inayoonesha tarehe ambayo mizani husika ilihakikiwa pamoja na tarehe ya mwisho ambayo stika hiyo itakuwa imekoma matumizi yake.

“Kwahiyo mwananchi akiiona ile stika inampa uhakika kuwa mizani hiyo imehakikiwa na WMA,” alisisitiza Kajungu. Kuhusu ufungashaji wa mazao ya shamba, alieleza kuwa kwa mujibu wa sheria, kufungasha mazao ya shamba kwa uzito unaozidi kilo 100 unatafsiriwa kama lumbesa ambayo ni kosa kisheria.

Kajungu ametoa wito kwa wakulima na wananchi kwa ujumla kufahamu kwamba mazao yote ya shamba ni lazima yafungashwe kwa uzito unaokubalika kisheria ambao ni kilo 100.

Kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya vipimo Sura Na. 340, Kajungu alisisitiza umuhimu wa kuwepo vituo vya kununulia mazao ambavyo ni rahisi kuweka mizani iliyohakikiwa na WMA ili itumike kwa wakulima kuhakiki mazao yao.

Alisema itasaidia kujiridhisha kwamba yamefungashwa katika uzito wa kilo 100 bila kuzidi ili kupata faida stahiki kwa pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi.

Wataalamu wa Wakala wa Vipimo wanashiriki katika Maonesho ya NaneNane kitaifa jijini Dodoma na kikanda katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla.