January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara wakutana Dar,kujadili hali ya biashara

 

Na Bakari Lulela,Timesmajira

UMUIYA ya Wafanyabiashara Nchi (JWT) imesema kuwa licha ya hali ya biashara nchini kuwa nzuri na kuzidi kuimarika lakini bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara.

Hayo yameelezwa leo Novemba 25, 2024 na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa Kagera na Kanda ya Ziwa, Nicholaus Basimaki, wakati akisoma risala katika Mkutano Mkuu wa 10 wa JWT wa mwaka 2024 kwa niaba ya Wafanyabiashara Tanzania.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo ni pamoja  na Kodi ya ongezeko la thamani (VAT), tozo za ushuru wa Huduma asilimia 0.3 (Service Levy) na changamoto ya vibali na ukaguzi magetini na mipakani.

“Changamoto nyingine ni kuisha kwa muda wa matumizi kwa mashine za EFD’S. Wafanyabiashara wamelalamika suala la mashine za EFD’s kuisha muda wa matumizi baada ya miaka mitano.

“Hali hii huongeza gharama za uendeshaji biashara na kuwaumiza wafanyabiashara, hivyo ili kupunguza mzigo wa gharama zisizo za lazima kwa wafanyabiashara tunapendekeza mashine hizi zisiwe na muda wa ukomo wa matumizi pia zitolewe bure na TRA kwani ni moja ya kitendea kazi muhimu sana katika sekta ya biashara,” amesema.

Ameongeza kuwa, pia changamoto nyingine ni utitiri wa kodi na watoza kodi, kodi ya VAT kukusanywa kwa mfumo wa makadirio badala ya risiti za mauzo, matumizi ya nguvu kwenye ukusanyaji wa kodi, kodi ya Zimamoto na uwepo wa vyombo viwili vyenye mamlaka sawa katika Nchi Moja (TRA na ZRA).

“Changamoto nyingine ni gharama za mabango ambapo zimelakamikiwa kuwa kubwa na za kuumiza kwani mfumo wa Sasa wa kulipia mabango hayo unaangalia ukubwa wa bango husika. Aidha wanasema kuwa mabango ni muhimu kwani yanasaidia wafanyabiashara kuvutia wateja ambao huwaingizia pato na kuwawezesha kulipa Kodi mbalimbali za serikali.

“Hivyo tunapendekeza kuwa mabango yaondolewe kodi au iwekwe bei elekezi ambayo italipika na siyo kutoza kulingana na ukubwa wa bango husika,” amesema.

Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za Wafanyabiashara nchini.

Ametoa wito kwa Taasisi zote za serikali zinazoshughulika na biashara nchini kuhakikisha zinaweka Mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara.

“Pia nitoe wito kwa wafanyabiashara mzidi kuimarisha ushirikiano uliojengeka baina yenu na Wizara kwani hakuna mfanyabiashara atakae nyanyasika kwa namna yoyote ile,” amesema Kigahe.

Awali Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema wataendelea kushirikiana na wafanyabiashara na tayari wameanza kushughulikia changamoto zao mbalimbali.

“Pia nitoe pole kwa waathirika pale Kariakoo, tutatumia sheria tulizo nazo kuleta unafuu. Ni suala la kuwatambua na nimeshaagiza nipate majina yao ili kuona namna gani ya kuwasaidia waweze kuendelea na biashara zao,” amesema Kamishna Mwenda.