November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara wajivunia Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Kisarawe

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Taifa (JWT), Hamis Livembe, amewataka wafanyabiashara Tanzania kufanya kazi kwa bidii kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi kiuchumi.

Amesema wana wajibu wa kujivunia juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kushughulikia kero zao na kufungua milango ya majadiliano jambo ambalo halikuwahi kufanyika miaka ya nyuma.

Livembe ameyasema hayo leo, wakati akizungumza na wafanyabishara wilayani Kisarawe mkoani Pwani, katika mwendelezo wa ziara za viongozi wa JWT kusikiliza kero za wafanyabiashara nchi nzima.

Amesema awali wafanyabishara walikuwa hawana nafasi ya kusikilizwa isipokuwa wakati inapotokea migomo na maandamano lakini tangu utawala wa Rais Samia, wamepewa nafasi ya kujisemea na kusikilizwa.

“Tutembee kifua mbele, tufanye biashara kwa amani na utulivu, bila kusahau kutimiza wajibu wetu. Tumekutana hapa leo tujadili matatizo yetu kipi kinatukwamisha kufanya biashara kwa utulivu ili kwa kushirikiana na serikali tukae meza moja na tuyamalize,” amesema Livembe.

Ametolea mfano wa moja ya kero ambazo imefanyiwa kazi ni faini ya kutokutoa risiti kwa mteja au kutoandika jina ambayo awali ilikuwa Sh. milioni 4.5 lakini imeshushwa hadi Sh. 1.5 baada ya wafanyabishara kulalamika.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Uongozi ya JWT, Ismail Masoud, amesema katika mikoa 12 waliyopita wamesikiliza kero nyingi ambazo sinafanana na tayari nyingine zimeanza kufanyiwa kazi.

Nao wafanyabiashara wa Wilaya ya Kisarawe, walilalamikia kodi za kero zinazotozwa na halmashauri na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwamo ya jengo la fremu anayotozwa mpangaji badala ya mwenye nyumba.

Ziara hiyo inaendea leo katika wilaya za Kibiti na Mkuranga mkoani humo.