Na Mwandishi wetu,Pwani
WAFANYABIASHARA wa soko la Bwilingu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani wametakiwa kuzingatia utunzaji na usafi wa mazingira katika soko hilo.
Wito huo umetolewa Juni 29,2024 na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe wakati wa uzinduzi wa soko la Bwilingu.
Dk Kapologwe amesema miundombinu ya soko la Bwilingu ni mizuri hivyo Wafanyabiashara wana jukumu la kufanya usafi wa mazingira na kuilinda miundombinu hiyo.
“Miundombinu iliyojengwa katika soko hili inalenga udhibiti wa taka ngumu pamoja na taka miminika,katika eneo hili mnaweza kujenga vyoo ambavyo vinatumiwa na wafanyabiashara wa soko hili,” amesema.
Ameeleza kuwa kampeni ya Mtu Ni Afya, yenye kauli mbiu ya ‘Fanya kweli,usibaki nyuma’ imejikita katika suala la usafi wa mazingira pamoja na usafi wa mtu mmoja mmoja kama unawaji wa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka.
Dkt. Kapologwe amesema pia kampeni hiyo imekuja kuhamasisha jamii suala zima la kufanya mazoezi.
“Mazoezi yanasaidia katika kuimarisha mwili na kupambana dhidi ya magonjwa ambayo sio ya kuambukiza ikiwemo kisukari,shinikizo la damu, ” amesema.
Amemuagiza Mwenyekiti wa soko la Bwilingu Shabaan Saidi kutengeneza sehemu maalumu ya kunawia mikono kwa wafanyabiashara na watu mbalimbali wanaofika katika soko hilo.
Katika hatua nyingine,Dk Kapologwe ameitaka jamii kuzingatia ulaji ulio bora na kuepuka suala la kutumia sukari nyingi katika chakula.
Naye Mkurugenzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Ramadhani Possi amesema kampeni ya Mtu Ni Afya,imewasaidia a katika kuhamasisha kampeni ya kunawa mikono kwa maji tiririka ambayo halmashauri hiyo ilikuwa imeanzisha kampeni hiyo.
Amesema Halmashauri yao imetumia kiasi cha milioni 90 katika ujenzi wa vyoo vya kisasa katika soko la Bwilingu pia imenunua gari maalumu la kubebea takataka kwa ajili ya kufanya usafi na utunzaji wa mazingira.
Mratibu wa Afya,Uzazi na Mtoto Wilaya ya Chalinze Beatha Mchopa amehimiza wafanyabiashara kwa ujumla pamoja na wakazi wa Wilaya ya Chalinze kuwa na utaratibu maalumu wa kunawa mikono.
Akielezea kuhusu hedhi salama,Mchopa amewashauri wazazi kujenga utaratibu malumu wa kuwafundisha watoto wao kuhusu hedhi salama.
“Watoto wanapokuwa katika kipindi cha balehe, wanatakiwa kujifunza namna gani ya kuishi katika hedhi salama,walimu shuleni pamoja na wazazi watambue mtoto anapoingia kwenye hedhi anatakiwa kutumia kitambaa salama na anatakiwa kujua jinsi ya kuhifadhi hivyo vitambaa na kukusanya na kuchoma moto,” amesema.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake