December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wafanyabiashara Igunga wamuangukia Mbunge

Na Lubango Mleka, Timesmajira Online,Igunga

WAFANYABIASHARA wa Soko la Magharibi Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Igunga Nicholas George Ngassa kuingilia kati mgogoro wao na Ofisa Biashara wa Wilaya hiyo juu ya malimbikizo ya ushuru wa soko kiasi cha shilingi 180,000 kwa kila mfanyabiashara sokoni hapo.

Hayo yamebainishwa na Wafanyabiashara hao wakati wa mkutano baina yao na Mbunge wa Jimbo hilo uliofanyika katika uwanja wa Soko la Magharibi lililopo Kitongoji cha Magharibi Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga.

“Tulipokea tangazo ambalo linataka tulipe sh. 180,000 kwa mkupuo, tukajiuliza ushuru ni nini? ushuru ni kwamba unapokutwa katika meza yako unatakiwa kulipa sh. 500 kwa wakati huo, mpaka hapa napo ongea hakuna mwakilishi wa Halmashauri aliyekuja kuomba ushuru ndani ya soko akanyimwa, tulipopata pigo hili la kulipa kwa wakati mmoja limetuchanganya,”amesema Sombe.

Huku Deus Gedi ameomba soko hilo eneo la jengo kuu kuwekewa umeme kwani taa za umeme jua ambazo Mbunge Ngassa alitoa hazitoshelezi ili Wafanyabiashara waweze kuuza bidhaa zao mpaka majira ya saa nne usiku.

Kwa upande wake Barozi wa mtaa wa Mbagala B-2 Josephat Mazezele amesema kuwa, kukosekana kwa barabara za uhakika kwenye mitaa katika eneo lake kumesababisha wajawazito wengi kujifungulia nyumbani nyakati za usiku japo wapo nje kidogo ya mji.

Huku Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magharibi Makalanga Mbongo, akiomba kujengwa kwa kituo cha mabasi yaendayo vijijini katika eneo ambalo Mbunge aliahidi pamoja na soko la mtaa wa Mbagala B kwani wapo mbali sana na soko la Magharibi hali anayoeleza kuwa itawasaidia kuwainua kiuchumi wakazi wa eneo hilo.

“Kilomita mbili za barabara tulizopewa kitongoji chetu hazitoshelezi tunaomba tuongezewe hata kwa fedha za Jimbo tuchongewe barabaza zaidi, pia umeme jazilizi tunaomba tupewe kipaumbele,” amesema Mbongo.

Naye Diwani wa Kata ya Igunga Athuman Hussain Mdoe amebaisha kuwa eneo la Mbagala B limepimwa na TARURA kwa ajili ya kujenga barabara, lakini pia Halmashauri na watu wa urasimishaji walipima maeneo ya wananchi na kutenga kituo cha mabasi yaendayo vijijini pamoja na soko.

Hivyo kutokana na wananchi kujenga nyumba kwa kasi eneo la shule lilikosekana, amewaomba kukaa kikao na kuona namna ya kupata eneo kwa ajili ya ujenzi huo wa shule ya msingi.

Hata hivyo, Mbunge Ngassa amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo kuongozana na Ofisa Biashara,viongozi wa chama, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Magharibi ili kukutana na wafanyabiashara wa soko na kuona namna nzuri ya kulipa ushuru kwani serikali ina nia nzuri ya ukusanyaji wa mapato.

“Suala la kuwa na umeme ndani ya Soko nimelichukua nina ahidi kuwaletea nguzo mpaka hapa sokoni,niwaombe kupitia umoja wenu mfanye ‘wirering’ mifumo ya umeme),nitaongeza taa za umeme wa jua ili muendelee kufanya biashara kwa nyakati za usiku kwani soko hili ni kubwa kwa uuzaji wa samaki katika mji wetu wa Igunga Mjini,”amesema Ngassa.