Na Daud Magesa na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
TAASISI za umma mkoani Mwanza zimeahidi kuendelea ushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC),kuhakikisha jamii inafahamu majukumu yanayofanywa na taasisi hizo.
Ahadi hiyo imetolewa Desemba 13,2024,katika hafla ya usiku wa Waandishi wa Habari na Wadau wa Habari Mkoa wa Mwanza 2024,iliofanyika jijini hapa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,wadau hao wamesema tasnia ya habari ina mchango mkubwa katika mafanikio na maendeleo ya taasisi hizo za umma.
Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Kanda ya Ziwa, Richard Toyota,amesema hafla hiyo ni namna nzuri ya kutengeneza uhusiano baina ya taasisi za umma,sekta binafsi na vyombo vya habari.
“TIRA imepiga hatua tangu mwaka 2011 hadi 2020 ilikuwa ikichangia pato la taifa kwa asilimia 0.5,lakini mwaka 2023 sekta ya Bima imechangia asilimia 2.02, ni hatua nzuri na uelewa wa wananchi kuhusu bima umeongezeka.Asilimia 50 hadi 60 ya Watanzania wana ufahamu wa bima kupitia vyombo vya habari,”amesema Toyota.
Toyota amesema uelewa wa matumizi ya bima kwa Watanzania bado uko chini,ni asilimia 20 hadi 30 wanaotumia huduma hizo na hivyo changamoto hiyo inahitaji kutatuliwa ili ifikapo mwaka 2030 Watanzania asilimia 80 wawe wanatumia huduma za bima na kuifanya sekta hiyo kukua hadi kufikia asilimia 5.
“Sheria ya Bima ya Afya kwa wote Namba 13 ya Mwaka 2023, inamtaka kila Mtanzania awe na bima, kwa hili uelewa wa kuhamasisha Watanzania tunahitaji vyombo vyenye weledi kufanya hilo,”amesema.
Kwa upande wake,Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Mkoa wa Mwanza,Jarath Mushashu,amesema,“Wanahabari ni familia,tumeshirikiana nao tangu mfuko umeanzishwa na wametuwezesha kufika mbalimbali, bila wao hatuwezi kufika tunakohitaji kufika,”.
Amesema kwa sasa NHIF ina jukumu la kutekeza Sheria Namba 13 ya mwaka 2023 ya Bima ya Afya kwa Wote, baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge,Desemba mwaka huu,Pia Waziri wa Afya,Jenista Mhagama,atazindua vifurushi vya bima kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo kutoa ufafanuzi wa Toto Afya Kadi.
“Afya ni mtaji na bila afya hata ungekuwa na fedha kiasi gani bado ni bure,ili nchi izalishe lazima watu wawe na afya bora na uhakika wa matibabu,watu wakate bima na kuchangiana kabla ya hujaugua ni vema,tusaidieni kufikisha elimu kwa jamii ili kujiunga na mfuko,”amessma Mushashu.
Kwa mujibu wa takwimu asilimia 15 ya Watanzania waliokuwa wanatumia bima ambapo CHF asilimia 6,NHIF asilimia 8 na bima zingine asilimia 1.3,hivyo mipango ya serikali kila mmoja ajiunge awe na uhakika wa matibabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Eric Hamissi,amesema mabdiliko ya jina la kampuni yamelenga kutokana na na kazi wanazozifanya za usafirishaji wa abiria na mizigo baada ya kubainia jina la MSCL lilikuwa haliaksi kazi hizo.
“Tumebeba wigo mpana wa jina la nchi yetu,tumeenea katika maziwa makuu ya Victoria,Nyasa na Tanganyika ambapo dira yetu 2025, ni kwenda hadi Bahari ya Hindi,tutajenga meli kubwa ya mizigo, tutaanza na meli mbili kwanza baada ya upembuzi yakinifu tujue ni meli ya aina gani tunapaswa kujenga,”amesema Eric.
Eric amesema,baada ya kuzaliwa mtoto mpya,wameanza na nyumbani,hivyo amewaomba waandishi wa habari watumie kalamu zao kuitangaza na kuiunga mkono TASHICO,ili kuiwezesha kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji kwa kutumia meli.
“Tunawashukuru waandishi wa habari kwa namna tunavyoshirikiana tangu kampuni ilipodorora,kwa umuhimu wake wa kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo ya maziwa makuu.Serikali iliwekeza ili kufufua na kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji kwa abiria na mizigo baada ya kujenga meli katika maziwa makuu,”amesema.
More Stories
NHIF yarejesha Toto Afya Kadi ,yazindua vifurushi vipya
Wanafunzi Tusiime waanza ziara nchini Uturuki
Wapeni kipaumbele wasichana kusoma sayansi