Na Mwandishi wetu ,Mpwapwa
WADAU mbalimbali wa Maendeleo wametakiwa kushirikiana na Serikali kuandaa mazingira rafiki kwa Wazee kukutana kuweka mipango mbalimbali ya Maendeleo.
Wito huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwanaidi Ali Khamis wakati akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dodoma katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Wazee yaliyofanyika Kimkoa Wilayani Mpwapwa mkoani humo.
Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa Wazee wanakuwa wapweke kwa kukosa maeneo ya kuwakutanisha na kubadilishana mawazo na uzoefu katika mazingira mbalimbali wanayoishi.
Amesema miongoni mwa mambo ambayo Wazee wanatakiwa kupewa kipaumbele ni mawasiliano hasa wakati huu wa mabadiliko ya teknolojia.
“Makundi haya hayapati fursa ya kunufaika na teknolojia au mara nyingi hayanufaiki katika fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia. Hivyo, kama nchi tunao wajibu wa kuhakikisha wazee wanapata fursa sawa” amesema Mwanaidi.
Ameongeza pia bajeti ya Afya imeongezeka ili kusaidia kuboresha huduma kwa wazee ikiwemo huduma za afya kutoka sh. bil 31 hadi bil. 270.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesisitiza jukumu la kuwatunza Wazee ni la familia na Jamii.
Ametoa wito kwa Jamii kuwakemea wale ambao hawatunzi Wazee wao na ikitokea mzee hana mtu wa kumhudumia Serikali imeweka utaratibu wa kuweka makao na hivi sasa kuna makao 13 nchini.
“Tusipowatunza wazee ni dhambi kubwa, utakuta mzee ana watoto wengi lakini wanashindwa kumtunza pamoja na kuwa na uwezo huo.
Serikali itatimiza wajibu wake lakini Jamii ina wajibu wa kwanza” amesisitiza Jingu.Ameongeza pia mabaraza ya wazee ni fursa muhimu ya Wazee kukutana na kujadili masuala yao ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto ya upweke, hivyo yatumike vizuri.
Kupitia risala yao iliyowasilishwa na mwenyekiti wa wazee Mkoa wa Dodoma mchungaji Petro Mpolo wameishukuru Serikali kwa kukamilisha zoezi la uundaji wa mabaraza ya wazee katika ngazi zote ambapo kilichobaki ni kuunda Baraza la Mkoa.
Aidha wameshukuru utaratibu uliowekwa na Waziri wa Afya wa kutoa huduma kwa Wazee kwa njia ya mtandao kila Jumamosi ambapo wanasikilizwa changamoto zao na kutafutiwa ufumbuzi.Â
Wazee hao walibainisha changamoto mbalimbali zinazotokana na uzee na kuomba Serikali iharakishe kuzifanyia kazi ikiwemo upatikanaji wa kadi za matibabu, upungufu wa dawa, kutoshirikishwa kwenye vikao vya maamuzi na kusumbuliwa na magonjwa kama tezi dume.
Aidha, wameiomba Serikali kusimamia utekelezaji wa maagizo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo Wazee kuelewa umuhimu wa kadi ya bima ya afya.
Maadhimisho hayo ya siku ya Kimataifa ya Wazee hufanyika kila Oktoba Mosi, ambapo mwaka huu yamefanyika katika ngazi ya Mkoa yakibebwa na Kaulimbiu: “Matumizi Sahihi ya Dijitali kwa Rika zote,”
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini