December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau waombwa kufadhili sekta ya elimu

Na Agnes Alcardo, Times Majira online Dar es Salaam.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angela Kairuki, ametoa wito kwa wadau wa elimu nchini, kutoa ufadhili katika masuala ya elimu msingi, kupitia Ushirika wa Kimataifa wa Kusaidia Maendeleo ya Elimu Duniani katika Nchi zinazoendelea GPE.

Waziri huyo ametoa wito huo Agosti 14,2023 Jijini Dar es Salaam alipokutana na wadau mbalimbali na viongozi wa Serikali wa Mkoani humo, kujadili namna ya kuweza kusaidia kupande wa elimu.

” Lengo la kukutana hapa ni kujadili na kuangalia ni namna gani tutaweza kuisaidia sekta ya elimu kupitia ushirika huu wa GPE, nimatumaini yangu wadau wote mliofika hapa mtafuata vigezo na masharti katika uandikaji wa barua zenu ili muweze kufadhili kwa kutoa misaada katika upande wa elimu msingi,” amesema Kairuki.

Aidha akizungumzia juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maeneo na mkakati wa serikali katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa zaidi ,amesema imekuwa mshirika na mnufaika wa Ushirika wa Kimataifa wa Kusaidia Maendeleo ya Elimu Duniani (GPE) tangu mwaka 2013, ambapo hadi sasa nchi imeshanufaika na ufadhili katika awamu mbili, huku alizitaja kuwa awamu ya kwanza ilianza mwaka 2014 hadi 2018.

Ambapo, Tanzania ilipokea kiasi cha dola za Kimarekani milioni 94.8 zilizolenga kukuza stadi za kusoma,kuandika na kuhesabu.

Ameongeza kuwa, pamoja na mafanikio haya kutokana na ufadhili wa GPE,serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu nchini ikiwemo ujenzi wa miundombinu.

Ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23 kiasi cha zaidi ya bilioni 296 (296,737,511,281.00) kutoka Serikali Kuu, kilipelekwa kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 11,611 katika shule kongwe za msingi na sekondari, ukamilishaji wa maabara za sayansi 291,mabwalo 86,mabweni 461, ujenzi wa uzio shule maalum 99, nyumba za walimu 298 (3 in 1) na matundu ya vyoo 9,700 katika Shule shikizi (Satelite Schools).

Pia amesema,kupitia ufadhili wa GPE Multiplier, zipo nchi 18 zimeweza kutengewa Dola za Kimarekani Mil50 kiwango cha juu cha mgao kwa mwaka 2023, ikiwa Tanzania ni mojawapo kati ya nchi hizo.

Huku ikielezwa kuwa, endapo Tanzania itaweza kupata ufadhili huu, fedha zake zitachangia katika kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango mipya iliyoibuliwa na mabadiliko ya Sera na Mitaala ya Elimu, hususan katika kufanikisha utekelezaji wa eneo la mafunzo ya amali.