November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau walivyoungana kuendeleza mbegu za asili

Na David John timesmajiraonline

Imeelezwa kuwa kumekuwa na dalili mbalimbali zinaonesha mbegu za asili za wakulima kutoweka kama hazitatafutiwa njia sahihi ya kuzitunza na kuzilinda hivyo itafika mahali ambako hakutakuwa na uhuru wa chakula.

Ambapo uhuru wa chakula unategemea uwepo wa mbegu za uhakika kwa wakulima,hivyo katika kunusuru hali hiyo kumekuwa na majadiliano yanayoendelea katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Huku sehemu kubwa ya majadiliano hayo yanahusu namna nzuri ya kuendeleza mbegu za asili ambazo zinatumiwa na wakulima na katika kunogesha majadiliano tayari shirika lisilo la kiserikali la Afsa la nchini Uganda limekuja na mapendekezo kadhaa yanayoonesha kuwa yakifuatwa na kutekelezwa upo uwezekano wa mbegu za asili za wakulima kuendelea kuwepo na kutumika.

Mraribu wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tabio Abdallah Ramadhan Mkindi alifafanua jambo kuhusu tafiti na mapendekezo yaliyotokana na tafiti zilizofanywa na shirika lisilola la kiserikali la Afsa kuhusu na kuwa na uhuru wa chakula barani Afrika .

Hata hivyo katika mapendekezo hayo wadau wakubwa katika sekta ya kilimo nchini Tanzania wametoa maoni na ushauri kuhusu uendelezwaji wa mbegu za wakulima kwa maana ya mbegu za asili.Mratibu wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya TABIO Abdallah Ramadhan Mkindi anaeleza kuwa mapendekezo ya AFSA na kwa mtazamo wake yamekuja wakati muafaka.

“Katika kuhamasisha masuala ya kuwa na uhuru wa chakula barani Afrika,moja ya maeneo muhimu ya kuzungumzia ni katika mfumo wa mbegu unaomilikiwa na wakulima, ambapo tafiti zimefanyika katika ngazi ya Afrika zinaonesha karibia asilimia 80 ya mbegu ambazo wakulima wamezitumia zinatokana na mfumo wa mbegu zinazomilikiwa na wakulima wenyewe,”anaeleza Mkindi na kuongea kuwa

“Kwa hapa Tanzania tafiti zimefanyika na zinaonesha mfumo huo unachangia zaidi ya asilimia 60 kwa baadhi ya mazao huku mazao mengine kwa asilimia asilimia 90 pia yapo mazao yanayotokana na mfumo huo kwa asilimia 100,”.

”Mkindi anaeleza kuwa mfumo huo unategemewa kama chanzo cha mbegu kwa wakulima hasa wadogo na unachangia upatikanaji wa pembejeo kwa kiasi kikubwa ambazo wakulima wanazitumia lakini haujawekewa mkakati wa kutosha kulinda mifumo iliyopo ili isipotee.

“Sera ya kilimo inaonesha mfumo huu haujatajwa wazi kama ni moja ya chanzo cha pembejeo ambazo wakulima wanazitegemea pia kwenye sheria yetu ya mbegu ya mwaka 2003 na sheria ya mwaka 2014 mfumo wa mbegu za mkulima haujatajwa,”.

Hivyo inakuwa ngumu kwa Serikali kuweka mipango au kanuni za kusimamia ndiyo maana wenzetu wa Afsa wameandaa mfumo huu pendekezwa wa kusimamia,kutambua na kuhamasisha mfumo wa mbegu zinazomilikiwa na wakulima na kulinda viumbe hai ili usipotee.

”Serikali na wadau waupitie mfumo uliopendekezwa na Afsa ili waone kwani lengo ni kutambua kwa kiasi gani na Watanzania wanaweza kuandaa mfumo wa kusimamia mbegu za mkulima ili zisipotee ambazo ndio chanzo kikubwa kinachotegemewa msimu mmoja mpaka mwingine.

Mkindi anaeleza kuwa mbegu za mkulima zikipotea athari yake ni kubwa, kwanza kwenye upatikanaji wa aina ya vyakula ambavyo walaji wanavitegemea na wanavitaji.

“Kuna magonjwa mengi yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, moyo , presha, na mengine ambayo yanatokana na ulaji mbovu au kula vyakula ambavyo sio salama hivyo mfumo huo wa mbegu za wakulima unawawezesha wakulima na walaji kupata vyakula vya kujenga afya kwa maana ndani yake vina lishe lakini pia kujitosheleza kwa chakula,”.

Aidha anaeleza kuwa tafiti ambazo zimefanyika maeneo mbalimbali nchini hapa hasa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na ile mikoa inazalisha chakula kingi hasa mahindi inaonesha kuwa bado mikoa hiyo inaongoza kuwa na utapia mlo kwa watoto wadogo.

Anataja athari nyingine ni upotevu wa viumbe hai vya mbegu za mkulima,Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinautajiri mkubwa wa viumbehai ambayo inashika nafasi ya juu duniani.

Hivyo hizo mbegu zikipotea maana yake tunapoteza na viumbehai na hizo mbegu ni chanzo kikubwa cha kupata vinasaba ambavyo watafiti wanavitegemea kwa ajili ya kuboresha mbegu.

Akizungumzia suala la uanzishwaji wa benki ya mbegu za mkulima, anasema tayari zimeanzishwa na zinaendelea kuanzshwa kwenye mikoa tofauti tofauti kwani kumekuwa na jitahada za mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yaanzisha benki za mbegu.

“Lakini kuanzisha benki bila maarifa utaweka mbegu lakini zitakufa, lazima benki hizo zikianzishwa wanaozisimamia wapewe elimu na maarifa yanayostahili kusimamia benki hizo za mbegu hivyo itakuwa sehemu rahisi ya wakulima kupata mbegu pia anaweza kuzitumia kwa kuzalisha kwa ajili ya wengine wanaohitaji wakazipata, wadau kama vituo vya utafiti wanapozihitaji kwa ajili ya utafiti benki za mbegu ni sehemu sahihi ambapo wanaweza kuzipata kwa ajili ya matumizi ya hizo mbegu,”.

Sanjari na hayo anaeleza kuwa katika wasilisho ambalo wamelifanya walipokutana na Kamati ya Bunge ,Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo walianisha benki nyingi ambazo zimekwisha aanzishwa mfano Mkoa wa Arusha na hiyo inatokana na jitihada zinazofanyika.

“Benki za mbegu za jamii 10 zimeanzishwa mkoani Arusha,Morogoro benki tatu, Lindi na Mtwara kuna benki saba, Shinyanga kuna benki mbili, Songwe benki mmoja na bado kuna zingine zinaendelea kuanzishwa sababu wakulima na jamii wamehamasika kuzianzisha benki hizo,baadhi ya mbegu zinasimamiwa kwa karibu na Maofisa Ugani na kituo cha taifa cha kuhifadhi vinasaba kilichopo Arusha,”.

Kwa upande wake Paul Chileo ambaye ni Ofisa Ufuatiliaji, Tathimini na Ushawishi kutoka Taasisi ya Kilimo Endelevu(TOAM) amesema dunia kwa sasa inataka maendeleo endelevu na kilimo kinabeba watu wengi na hasa Afrika.

“Bila kuwa na kilimo endelevu kwanza tutakuwa na tatizo kubwa dunia,tunataka kuboresha mifumo ya chakula na kama mnajua kuna mkutano mkubwa unaohusu masuala ya kilimo, huwezi kubadilisha mfumo wa chakulaukawa endelevu bila kuwa na mjadala na kuchukua hatua kwenye mbegu ambazo zinamilikiwa na wakulima kwani zina mchango mkubwa kwenye usalama wa chakula,”anasema.

Aidha anasema katika kuhakikisha lishe inapatikana watunga sera wanapaswa kutambua mapendekezo yalioletwa na Afsa ambayo yatafanya kuwe na mifumo ya chakula endelevu kwani kuna mikoa ambayo inazalisha zaidi lakini ndio inayoongoza kuwa na utapia mlo.Mfano wana mbegu ambazo zinaweza kuwasaidia kutatua tatizo la lishe na utapia mlo lakini ukisikiliza mbegu zinazopigiwa chapua hazileti suluhisho la kuzalisha chakula ambacho kitakuwa kina lishe hivyo hiyo ni changamoto.

“Ndio maana siku hizi watu wanatafuta dawa za nguvu za kiume lakini kuna vyakula ambavyo ni zaidi ya dawa za hizo , kwa hiyo kitu cha kwanza kutambua ukiangalia mapendekezo yote yana lengo la kuleta mfumo wa chakula endelevu, kuna changamoto kubwa kwenye mifumo yetu ya chakula ambapo watalaam wanasema inabidi tuondoe ukoloni mamboleo,Afrika tunafikiria tunachangamoto ya utapia mlo lakini suluhu haitoki ndani na wakati mwingine inapotoka nje inakuwa sio endelevu ambayo inaleta mabadiliko yanayotakiwa,”.

Ameongeza unakuta chakula kinachozalishwa inabidi kikafanyiwe uchunguzi, lakini kuna mbegu ambazo zinaweza kuzalisha na zikatoa mchango mkubwa kwenye kutatua tatizo la lishe kwa hiyo ukiangalia yale mapendekezo ya Afsa kwa kiwango kikubwa yanataka kuja na suluhu ya kudumu.

Ametoa mfano wanataka kutengeneza kamati ya kitaifa ambazo zitatambua mbegu zetu zipo na zipo kwenye hali gani na zinaendelezwaje,baada ya hapo kuzilinda na kuziendelezo sasa wanakuja na mapendekezo ya mikoa lakini kuna maeneo ya kiasili.

Hivyo anasema ni vizuri kushirikisha benki za asili katika mfumo huo wa kuzilinda na kuziendeleza mbegu na wakulima washiriki kikamilifu na usiwe mfumo wa watalaamu peke yao na wakulima peke yao.

“Tunachotaka ni kuona mtandao mzima wa wakulima unashirikishwa na kupewa kipaumbele kwenye vituo vya utafiti.” Mwisho