January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wajadili uwakilishi wa mwanamke katika siasa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Bukoba

SHIRIKA la Omuka Hub kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Marekani National Democratic Institute – (NDI) wameandaa majadiliano ya Jukwaa la Wanawake katika siasa, kujadili mapendekezo ya kikosi kazi na maazimio ya mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika Septemba 11 hadi 13, 2023 mkoani Dar es Salaam.

Majadiliano hayo yameandaliwa chini ya uratibu wa Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira wilayani Bukoba mkoani Kagera ambapo amesema lengo ni kuunga mkono maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uwakilishi wa wanawake kwenye siasa.

“Mjadala juu ya ushiriki wa wanawake katika siasa katika ngazi zote kuanzia kitongoji hadi Taifa umefanyika Bukoba Mjini na umehudhuriwa na washiriki 100 kutoka makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo viongozi wa dini, siasa, wanawake viongozi , wakuu wa mashirika/NGOs na wengine.

Lugangira amesema maazimio ya mjadala huo yanakwenda kuwa chachu katika utekelezaji wa maono ya Rais Samia ya kuimarisha uwakilishi wa wanawake katika siasa ambayo yatawasilishwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kupitia Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika majadiliano hayo.

“Washiriki wa semina hii wamempongeza Rais Samia kwa hotuba nzuri aliyotoa wakati anafungua mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa kwani imeeleza uhalisia na inatoa dira jinsi ambavyo shughuli za siasa zinapaswa kufanyika nchini ili kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa,” amesema.

Kwa upande wake Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza amempongeza Mbunge Lugangira kwa ubunifu wa kuandaa majadiliano hayo kwa ngazi ya jamii ambapo amefurahia kukutana na washiriki kutoka ngazi ya jamii ambao wameonesha uelewa mkubwa wa masuala ya ushiriki wa wanawake katika siasa huku akisema kuwa maoni yao amechukua na yatafanyiwa kazi.

Msajili Msaidizi Nyahoza ametumia nafasi hiyo kuliomba shirika la NDI kuendelea kushirikiana na Mwanziishi wa Shirika la Omuka Hub ili mafunzo hayo yafike kila kona ya nchi.