Na.Judith Ferdinand
Miongoni mwa changamoto zinazozikabili Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini ni pamoja na halmashauri nyingi kutokuwa na uwezo wa kuandaa maandiko ya miradi yanayokidhi vigezo vya kupata fedha au kukopesheka.
Pamoja na kutokuwa na rasilimali fedha za kutosha kutoka vyanzo vya ndani ili kutekeleza mipango mikakati ya maendeleo ya kila mwaka.
Katika kuhakikisha miradi mikakati ya halmashauri inatekelezwa kikamilifu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya waliandaa Kongamano la Majadiliano juu ya mada zinazohusu utekelezaji wa mipango mikakati ya halmashauri nchini.
Ambapo majadiliano hayo yalifanyika kwa siku mbili jijini Mwanza Machi 9 hadi 10 mwaka huu, kupitia mradi wa Uendelezaji Miji (Green and Smart Cities ‘ _Sasa_ ” project) ambao nchini hapa unatekelezwa katika Halmashauri za Jiji la Mwanza na Tanga, na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Akiwasilisha mada katika majadiliano hayo ya siku mbili, Meneja Uendelezaji Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB), Joseph Felix Chilambo ameeleza kuwa halmashauri nyingi hazina uwezo wa kuandaa miradi inayokidhi vigezo vya kukopesheka.
Hata zikikopesheka hazirudishi fedha kwa wakati huku akitolea mfano wa benki hiyo,ambapo ameeleza kuwa benki hiyo hadi sasa imetoa kiasi cha bilioni 8 lakini fedha zilizorudishwa kati ya hizo ni bilioni 1.8 tu.
“Changamoto za Halmashauri katika kupata fedha za mikopo kutoka benki au taasisi za kifedha ni uwezo mdogo wa kuandaa mradi inayokidhi mahitaji ya kiufundi, kibiashara, kifedha, kijamii na kimazingira pamoja kutokuwa na usimamizi madhubuti wa hatua za utekelezaji wa mradi,” ameeleza Chilambo.
Ameeleza kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa kuangalia vyanzo tofauti tofauti vya fedha vya muda mrefu ikiwa ni pamoja na mikopo ya benki kwa ajili ya kutekeleza miradi ya halmashauri nchini.
“Uratibu sahihi wa mipango na wadau mbalimbali kwenye miradi yenye manufaa ya kibiashara inapaswa kufadhiliwa kupitia vyanzo vya kibiashara kama mikopo ya benki, ushirikishwaji wa sekta binafsi (PPP), matumizi ya hati fungani za kimataifa au dhamana na vifaa kwa ajili ya utoaji wa huduma za umma zinazotarajiwa, “ameeleza Chilambo.
Kaimu Ofisa Muidhinishaji wa Mfuko wa EDF kutoka Wizara ya Fedha na Mpango, Jonathan Mpuya amekiri kuwa ni kweli kwamba watendaji wa halmashauri walio wengi wana uwezo mdogo wa kuandika maandiko ya mradi.
“Hilo ni moja ya eneo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi katika mradi wa Green and Smart Cities “Sasa” project,”ameeleza.
Mpuya ameeleza kuwa, mipango ya miradi iliyowasilishwa katika majadiliano hayo ni orodha tu ya miradi ambayo haijafanyiwa upembuzi yakinifu,hivyo hali hiyo inaonesha kuwa ni kweli uwezo katika halmashauri bado ni mdogo.
“Wizara ya fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Raisi – TAMISEMI tunachukua jambo hili kwa ajili ya kulifanyia kazi ili halmashauri ziweze kupata fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati na kutekeleza kama ilivyopangwa,”ameeleza Mpuya na kuongeza kuwa
Upungufu wa fedha za kutekeleza miradi katika halmashauri
Akizungumzia suala la upungufu wa fedha za utekelezaji wa miradi, Mpuya ameeleza kuwa kutokana na upungufu wa fedha za utekelezaji wa miradi ndio maana wameitisha kongamano hilo ili wadau wajadiliane kwa kina na kubuni mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Miongoni mwa wadau, walishirikishwa katika kongamano hilo ni kutoka katika taasisi za fedha, sekta binafsi, Taasisi za Elimu ya juu na Asasi zisizo za kiserikali kwani baadhi ya miradi siyo lazima itekelezwe na halmashauri kwani kwamba miradi mingine inaweza kutekelezwa na sekta binafsi.
“Miradi hiyo inatakiwa kuwa inafadhiliwa na fedha za halmashauri yenyewe lakini na vyanzo vingine vya mapato ambavyo vinaweza kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa, ndio maana tumewaita wadau watambue kuwa kuna fursa….., maana inawezekana katika uandaaji wa hii mipango, haikuwahusisha wadau wa sekta binafsi na taasisi za kifedha zione kuwa zinaweza kuingia katika kuunga mkono miradi na waone kuna fursa,”ameeleza Mpuya.
Nini hatua za serikali katika kuhakikisha mipango mikakati inatekelezwa
Mratibu wa Programu ya Uimarishwaji Mikoa na Serikali za Mitaa (RLGSP) kutoka TAMISEMI, Lemmy Shumbusho, ameeleza kuwa wamegundua halmashauri nyingi zinakosa uwezo wa uandaaji wa mipango mikakati ambayo inaweza kutekelezeka.
Licha ya changamoto hiyo, ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kwa kuwapa mafunzo watendaji wa halmashauri pamoja na kuandaa muongozo wa utekelezaji miradi.
Akifafanua kuhusu halmashauri kutokuwa na fedha za kutosha za kutekeleza miradi, anaeleza kuwa wamekuwa wakitafuta wadau, kuhamasisha miradi ya mashirikiano pamoja na kuhimiza halmashauri kuwekeza katika miradi inayolipa ili ijisimamie.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo cha Mipango Dodoma, Dkt.Titus Mwageni ameeleza kuwa uhamasishaji wa taasisi za fedha za mtaji ni muhimu sana kwani bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kidogo sana kwa madhumuni ya uwekezaji.
Dkt. Mwageni ameeleza kuwa kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuangalia ni namna gani mipango mikakati inaweza kutekelezeka vizuri ngazi za halmashauri ili kuleta tija ambapo halmashauri za Jiji, Manispaa na Wilaya ni taasisi muhimu katika kuleta maendeleo kwa wananchi wote nchini.
Ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto nyingi kwa halmashauri kushindwa kutekeleza mipango waliojipangia ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha, utaalamu wa namna ya kusimamia, uandaaji, utekelezaji na kufanya tathimini ya miradi kama ina matokeo chanya au lah.
Pia ameeleza kuwa lazima taasisi hizi ziweze kuwa na mipango mikakati mizuri ambayo imetekelezwa vizuri na kufanyiwa tathimini kwa kuona namna gani imeleta matokeo chanya.
“Halmashauri nyingi haziwezi kuwa na fedha za kutosha kuwekeza katika maeneo muhimu ya uwekezaji na hivyo sekta binafsi zinaweza kuwa suluhisho zuri katika uwekezaji unaopendekezwa,”.
Ameeleza kuwa changamoto ya ubia kati ya halmashauri na sekta binafsi ni uwepo wa masuala mengi ya kisera na kisheria yanayotokana na urasimu ambao mwisho wake huwakatisha tamaa wawekezaji binafsi kuunga mkono uwekezaji wa serikali katika halmashauri zetu nchini.
“Kuunda muongozo wa msingi wa takwimu na taarifa za uwekezaji wa kikanda au wilaya baada ya LGAS kupanga na kuteua maeneo ya uwezekano wa uwekezaji kunapaswa kuwa na kanzi-data ya miongozo ambapo taarifa zote za uwekezaji kwa halmashauri fulani zitakusanywa na kupatikana kwa wawekezaji na wadau wengine kutoka ndani au nje ya mamlaka,” ameeleza Dkt. Mwageni.
Suluhisho la halmashauri kutekeleza mipango mikakati
Dkt. Mwageni ameeleza kuwa suluhisho moja wapo ni halmashauri husika kuwajengea uwezo wa kitaalamu watumishi wake ya namna ya kuandaa mipango, kutumia mipango wakati wa kufanya utekelezaji pamoja na kufanya tathimini pia namna ya usimamiaji wa mipango kwa ujumla ili iweze kuleta matokeo.
Pia, halmashauri ziweze kuhakikisha ni namna gani zinatengenezewa miradi ya kupata fedha kutoka kwenye vyanzo vyao vya ndani kwani bila halmashauri kuwa imara kifedha haiwezi kutekeleza hiyo mipango.
“Halmashauri nyingi zimekuwa zikitegemea fedha kutoka Serikali Kuu, na kama tunavyoelewa serikali ina majukumu mengi, fedha hizo zimekuwa zikipungua kadri miaka inavyoenda,suluhisho ni halmashauri kuja na miradi ya kimkakati ya kuweza kupata fedha ili ziweze kupata fedha na kusimamia utekelezaji wa mipango hii kwani wanamipango mizuri ila wanakwanishwa na uhaba wa rasilimali fedha,”.
Vilevile ameeleza kuwa suluhisho jingine ni kushirikiana na sekta binafsi ambayo ni injini na chachu ya maendeleo kwa sababu inauzoefu mkubwa sana kwenye biashara.
“Halmashauri ikishirikiana na sekta binafsi kuanzisha miradi mbalimbali ya kibiashara, sekta binafsi itapata faida na italipa kodi kwenye halmashauri zetu na ikatumika kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kutekeleza mipango ya kimaendeleo ya halmashauri husika,”ameeleza.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Miji na Vijijini kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Rachel Kaduma ameeleza kuwa katika juhudi za serikali za kuhakikisha halmashauri inapata fedha, TAMISEMI imeboresha mifumo ya kukusanya mapato ambapo kwa sasa upo mfumo wa kieletroniki unaotambulika kama “Tausi” ambapo mapato yanakusanywa moja kwa moja kwa njia ya mfumo.”
Halmashauri inapokuwa na chanzo fulani cha kukusanya mapato moja kwa moja yanasomwa kwenye mfumo na tangu tumeanza kutumia mfumo huo wa Tausi kumekuwa na mafanikio ya mapato kwa kila halmashauri na miundombinu inaendelea kuimarishwa na kusaidia halmashauri kutekeleza mipango mikakati yao,” ameeleza.
Umuhimu wa sekta binafsi katika kutekeleza mipango mikakati ya halmashauri Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Myfish Tanzania company Ltd. Elipidius Mpanju, ameeleza kuwa sekta binafsi zinaweza kushirikiana na halmashauri kutengeneza mpango mikakati kwa sekta binafsi kuhusishwa moja kwa moja katika utungaji wa sera kwani moja ya mtekelezaji na mlaji ni sekta hiyo.
“Tukubaliane kwamba Serikali haiwezi kufanya vitu vyote,vingine vinaweza kufanywa na sekta binafsi na kuwapunguzia gharama na muda na ikafanyika kirahisi mathalani leo hii nikitaka kumtafuta mtaalam naweza kwenda nchi nyingine nikamchukua Mtaalam na kufanya naye kazi lakini serikalini lazima ufuate utaratibu wa unaochukua muda mrefu,”.
Meneja wa Programu ya Maendeleo ya Miji Umoja wa Ulaya Tanzania, Martino Vinci ameeleza kuwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya itaendelea kufadhili mradi huo na kuzitaka halmashauri zitumie fursa zilizopo kwa kushirikiana na sekta binafsi kuikamilisha mipango yao ya kimaendeleo licha ya changamoto wanazokabiliana nazo kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia