December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau waiweka Serikali mtegoni

Na Mwandishi Wetu

Mgeni Rasmi katika Kongamano la Wahariri na wadau wa uhifadhi, Mazingira na Utunzaji Vyanzo vya Maji, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Mwennyekiti wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Raasilimali na Taarifa (MECIRA) wakati konngamano hilo linaendelea katika ukumbi wa Masiti mkoani Iringa.

Serikali imetakiwa kufanya maamuzi magumu ili kuokoa chanzo cha maji cha Bonde la Ihefu ambalo limevamiwa na familia 12 na kusababisha chanzo hicho kukauka.

Akizungumza katika Kongamano la Wahariri wa Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji leo Desemba 19,2022 mkoani Iringa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kuwa inasikitisha kuona kwamba uharibifu wa mazingira ni wa kiwango cha juu huku zikiwepo familia 12 zinazojinufaisha kupitia Bonde hilo wakiendelea kukaliwa kimya.

Amesema kuwa ameamua kutoa taarifa hizo hadharani licha ya ukweli kuwa anajua wapo watu ambao hawatapenda kutokana na ukweli kuwa jambo hilo hata watendaji wa Serikali wanajua ila wamefunga midomo.

Balile amesema kuwa kama wahusika yaani watendaji wa Serikali hawatampatia orodha ya majina ya familia hizo yeye yupo tayari kufanya hivyo ili kunusuru chanzo hicho  ambacho kinaendelea kutokea kwa sasa.

Mwenyekiti huyo akaongeza kuwa familia hizo ndizo zinapaswa kunyweshwa sumu kabla  ya wengine kwa sababu wao ndio chanzo kikuu cha uhabifu huo na makusudi kabisa wamekuwa  wakifanya hivyo kwa manufa yao binafsi.

Mwenyekiti wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA), Habibu Machange kabla ya kumkaribisha Balile, amesema kuwa Tanzania ipo katika hatua mbaya ya uharibifu wa mazingira.

Akizungumza kwa hisia, Machange amesema hali hiyo ndiyo ambayo imechangia vyanzo vingi vya maji kukaua. Amesema kupitia ripoti ya mazingira, asilimia 16 ya ardhi ya Tanzania ni jangwa huku asilimia 63 ikiwa imeharibiwa.

“Mto Ruaha, Malagalasi, Ruvu, Ruvuma na mingine mingi kama hatua za haraka hazitachukuliwa tutavuna mabua,” amesema na kuongeza;

“Leo ni siku ya 130 mto Ruaha hautiririshi maji, sisi wanahabari hatutakuachia wewe jukumu la mazingira, tutakunywa sumu kwa ajili ya mazingira.”

Kulingana na Machange, Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanao uwezo mkubwa wa kusababisha maji ya Mto Ruaha kutiririka mwaka mzima tofauti na hali ilivyo sasa.