April 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau waitwa kuchangia upauaji Maabara sekondari ya Mtiro

 

Fresha Kinasa TimesMajiraOnline,Mara.

WADAU mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Wananchi wa Kata ya Bukumi Jimbo la Musoma Vijijini wameombwa kujitokeza kushiriki katika zoezi la harambee ya  uchangiaji wa fedha Shilingi Mil.25 zinazohitajika kwa ajili ya kupaua maboma ya maabara tatu za Masomo ya Sayansi za  Mtiro Sekondari yaliyokamilishwa shuleni hapo.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa juhudi zinazofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo Prof.Sospter Muhongo na Wananchi Jimboni humo kuhakikisha shule za Sekondari zinakuwa na maabara ili wanafunzi  wasome kwa vitendo masomo hayo ukiwa ni mkakati wa kuandaa  Wataalamu kwenye nyanja za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambao Taifa na  Dunia inawahitaji kuchochea maendeleo.

Hayo yameelezwa  kupitia Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo Aprili 10, 2025, ambapo imesema
“harambee ni Jumanne Aprili 22, 2025.
Gharama za upauaji ni Mil. 25. Harambee ya Mbunge ya kuezeka maboma hayo itapigwa shuleni hapo saa 8 mchana watu wote mnakaribishwa.” imeeleza taarifa hiyo. 

Mtiro Sekondari ipo Kata ya Bukumi yenye Vijiji vya Buira, Bukumi, Buraga na Busekera na ilifunguliwa mwaka 2006 Haina maabara hata moja.
Ambapo kwa Sasa inakamilisha ujenzi wa maabara 3 za masomo ya sayansi (physics, chemistry & biology laboratories)

Ambapo, harambee ya kupata vifaa vya ujenzi inayotarajia kufanyika ina malengo makuu ya kukamilisha ujenzi wa maabara 3 za masomo ya sayansi kwa kupaua Majengo hayo kwa Mil.25.

Pili Wanafunzi 672 kidato cha kwanza hadi cha nne kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo kwenye mazingira sitahiki na tatu kuanzisha “High School” ya masomo ya sayansi kwani bweni, maji na umeme vipo.

Wananchi wa Kata ya Bukumi akiwemo Shadrack Joseph wamesema harambee hiyo itakuwa na manufaa kuwezesha maboma hayo kukamilishwa ili kutimiza matarajio ya kuona Watoto wakisoma masomo ya Sayansi kwa Vitendo.